The Noble Qur'an Encyclopedia
Towards providing reliable exegeses and translations of the meanings of the Noble Qur'an in the world languagesStoneland, Rock city, Al-Hijr valley [Al-Hijr] - Swahili translation - Ali Muhsen Al-Berwani
Surah Stoneland, Rock city, Al-Hijr valley [Al-Hijr] Ayah 99 Location Maccah Number 15
Alif Lam Ra. (A.L.R). Hizi ni Aya za Kitabu na Qur'ani inayo bainisha. [1]
HUENDA ikawa walio kufuru wakatamani wange kuwa Waislamu. [2]
Waache wale, na wastarehe, na iwazuge tamaa. Watakuja jua. [3]
Na hatukuuangamiza mji wowote ule ila ulikuwa na muda wake maalumu. [4]
Hawawezi watu wowote kuitangulia ajali yao, wala kuchelewa. [5]
Na walisema: Ewe uliyeteremshiwa Ukumbusho! Hakika wewe ni mwendawazimu. [6]
Mbona hutuletei Malaika ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli? [7]
Sisi hatuwateremshi Malaika ila kwa sababu ya haki, na hapo hawatapewa muhula. [8]
Hakika Sisi ndio tulio teremsha Ukumbusho huu, na hakika Sisi ndio tutao ulinda. [9]
Na hakika tulikwisha watumia Mitume mataifa ya mwanzo. [10]
Na hakuwafikia Mtume ila walimkejeli. [11]
Na kama hivi ndivyo tunavyo ingiza katika nyoyo za wakosefu. [12]
Hawayaamini haya, na hali ya kuwa umekwisha wapitia mfano wa watu wa kale. [13]
Na lau tungeli wafungulia mlango wa mbingu, wakawa wanapanda, [14]
Basi wangeli sema: Macho yetu yamelevywa, bali sisi wenyewe tumerogwa. [15]
Na hakika tumeweka katika mbingu vituo vya sayari, na tumezipamba kwa wenye kuangalia. [16]
Na tumezilinda na kila shetani afukuzwaye. [17]
Isipo kuwa mwenye kusikiliza kwa kuibia, naye hufuatwa na kijinga cha moto kinacho onekana. [18]
Na ardhi tumeitandaza na humo tumeweka milima, na tumeotesha kila kitu kwa kiasi chake. [19]
Na tumekujaalieni humo vitu vya maisha yenu, na ya hao ambao nyinyi sio wenye kuwaruzuku. [20]
Na hakuna chochote ila asili yake inatokana na Sisi; wala hatukiteremshi ila kwa kipimo maalumu. [21]
Na tunazipeleka pepo za kupandishia, na tunateremsha kutoka mbinguni maji, kisha tukakunywesheni maji hayo. Wala si nyinyi mnayo yaweka. [22]
Na Sisi ndio tunao huisha na tunao fisha. Na Sisi ndio Warithi. [23]
Na tunawajua walio tangulia katika nyinyi, na tunawajua waliotaakhari. [24]
Na hakika Mola wako Mlezi ndiye atakaye wakusanya. Hakika Yeye ni Mwenye hikima na Mjuzi. [25]
Na tulimuumba mtu kwa udongo unao toa sauti, unao tokana na matope yaliyo tiwa sura. [26]
Na majini tuliwaumba kabla kwa moto wa upepo umoto. [27]
Na Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Hakika Mimi nitamuumba mtu kwa udongo unao toa sauti, unao tokana na matope yaliyo tiwa sura. [28]
Basi nitakapo mkamilisha na nikampulizia roho yangu, basi mumwangukie kumsujudia. [29]
Basi Malaika wote pamoja walimsujudia, [30]
Isipo kuwa Iblisi. Yeye alikataa kuwa pamoja na walio sujudu. [31]
(Mwenyezi Mungu) akasema: Ewe Iblisi! Una nini hata hukuwa pamoja na walio sujudu? [32]
Akasema: Haiwi mimi nimsujudie mtu uliye muumba kwa udongo unaotoa sauti, unao tokana na matope yenye sura. [33]
(Mwenyezi Mungu) akasema: Basi toka humo, kwani hakika wewe ni maluuni! [34]
Na hakika juu yako ipo laana mpaka Siku ya Malipo. [35]
Akasema (Iblisi): Mola wangu Mlezi! Nipe muhula mpaka siku watapofufuliwa. [36]
(Mwenyezi Mungu) akasema: Hakika wewe ni katika walio pewa muhula [37]
Mpaka siku ya wakati maalumu. [38]
Akasema: Mola wangu Mlezi! Ilivyo kuwa umenitia makosani, basi nahakikisha nitawazaini hapa duniani na nitawapoteza wote, [39]
Ila waja wako walio safika. [40]
Akasema: Hii Njia ya kujia kwangu Iliyo Nyooka. [41]
Hakika waja wangu, wewe hutakuwa na mamlaka juu yao, isipo kuwa wale wapotofu walio kufuata. [42]
Na bila shaka Jahannamu ndipo pahali pao walipo ahidiwa wote. [43]
Ina milango saba; na kwa kila mlango iko sehemu walio tengewa. [44]
Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na chemchem. [45]
(Wataambiwa:) Ingieni kwa salama na amani. [46]
Na tutaondoa chuki iliyo kuwamo vifuani mwao, wawe ndugu juu ya viti vya enzi wameelekeana. [47]
Humo hayatawagusa machofu, wala hawatatolewa humo. [48]
Waambie waja wangu ya kwamba Mimi ndiye Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. [49]
Na kwamba adhabu yangu ndio adhabu iliyo chungu! [50]
Na uwape khabari za wageni wa Ibrahim. [51]
Walipo ingia kwake na wakasema: Salama! Yeye akasema: Hakika sisi tunakuogopeni. [52]
Wakasema: Usiogope. Sisi tunakubashiria kijana mwenye ujuzi. [53]
Akasema: Mnanibashiria nami uzee umenishika! Basi kwa njia gani mnanibashiria? [54]
Wakasema: Tunakubashiria kwa haki; basi usiwe miongoni mwa wanaokata tamaa. [55]
Akasema: Na nani anaye kata tamaa na rehema ya Mola wake Mlezi ila wale walio potea? [56]
Akasema: Hebu nini amri yenu, enyi wajumbe? [57]
Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa kaumu ya wakosefu! [58]
Isipo kuwa walio mfuata Luut'i. Bila ya shaka sisi tutawaokoa hao wote. [59]
Ila mkewe. Tunakadiria huyo atakuwa miongoni watao bakia nyuma. [60]
Basi wale wajumbe walipo fika kwa Luut'i, [61]
Alisema (Luut'i): Hakika nyinyi ni watu msio juulikana. [62]
Wakasema: Bali sisi tumekuletea yale waliyo kuwa wakiyafanyia shaka. [63]
Na tumefika kwako kwa Haki, na hakika sisi tunasema kweli. [64]
Basi ondoka na ahli zako usiku ungalipo, nawe ufuate nyuma yao,wala yeyote kati yenu asigeuke nyuma. Na mwende mnapo amrishwa. [65]
Na tukamfunulia hukumu hiyo, ya kwamba hata wa mwisho wao hao ikifika asubuhi atakuwa kesha katiliwa mbali. [66]
Na wakaja watu wa mji ule nao furahani. [67]
Akasema: (Luut'i) Hakika hawa wageni wangu, basi msinifedheheshe. [68]
Na mcheni Mwenyezi Mungu, wala msinihizi. [69]
Wakasema: Sisi hatukukukataza usimkaribishe yeyote? [70]
Akasema: Hawa binti zangu, ikiwa nyinyi ni watendaji. [71]
Naapa kwa umri wako! Hakika hao walikuwa katika ulevi wao, wakihangaika ovyo. [72]
Ukelele ukawatwaa wakipambaukiwa. [73]
Na tukaigeuza nchi juu chini, na tukawanyeshea mvua ya mawe ya udongo wa Motoni. [74]
Hakika katika hayo zipo ishara kwa waaguzi. [75]
Na miji hii ipo kwenye njia inayo pitiwa. [76]
Hakika katika hayo ipo ishara kwa Waumini. [77]
Na Hakika watu wa kichakani, walikuwa wenye kudhulumu [78]
Kwa hivyo tukawaadhibu. Na nchi mbili hizi ziko kwenye njia iliowazi. [79]
Na bila ya shaka wakaazi wa Hijr waliwakanusha Mitume. [80]
Na tuliwapa ishara zetu, nao wakazipuuza. [81]
Nao walikuwa wakichonga majumba katika milima kwa amani. [82]
Basi ukelele ukawatwaa asubuhi. [83]
Hayakuwafaa waliyo kuwa wakiyachuma. [84]
Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ila kwa ajili ya Haki. Na hakika Kiyama kitafika. Basi samehe msamaha mzuri. [85]
Hakika Mola wako Mlezi ndiye Muumbaji Mjuzi. [86]
Na tumekupa Aya saba zinazo somwa mara kwa mara, na Qur'ani Tukufu. [87]
Usivitumbulie macho yako vitu tulivyo waneemesha makundi fulani kati yao, wala usiwahuzunikie. Na wainamishie bawa lako (la huruma) Waumini. [88]
Na sema: Hakika mimi ni mwonyaji mwenye kubainisha. [89]
Kama hivyo tuliwateremshia walio gawa, [90]
Ambao wakaifanya Qur'ani vipande vipande. [91]
Basi Naapa kwa Mola wako Mlezi! Tutawahoji wote. [92]
Kwa waliyo kuwa wakiyatenda. [93]
Basi wewe yatangaze uliyo amrishwa, na jitenge na washirikina. [94]
Hakika Sisi tunatosha kukukinga na wanao kejeli. [95]
Hao wanao fanya kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu yupo mungu mwingine.Basi, watakuja jua! [96]
Na Sisi tunajua kwa hakika kuwa wewe kifua chako kinaona dhiki kwa hayo wayasemayo. [97]
Basi mtakase Mola wako Mlezi kwa kumhimidi, na uwe miongoni wanaomsujudia. [98]
Na muabudu Mola wako Mlezi mpaka ikufikie Yakini. (nao ni Mauti) [99]