The Noble Qur'an Encyclopedia
Towards providing reliable exegeses and translations of the meanings of the Noble Qur'an in the world languagesThe Poets [Ash-Shuara] - Swahili translation - Ali Muhsen Al-Berwani
Surah The Poets [Ash-Shuara] Ayah 227 Location Maccah Number 26
T'aa Siin Miim. (T'.S.M.) . [1]
Hizi ni Aya za Kitabu kinacho bainisha. [2]
Huenda labda ukajikera nafsi yako kwa kuwa hawawi Waumini. [3]
Tunge penda tungeli wateremshia kutoka mbinguni Ishara zikanyenyekea shingo zao. [4]
Wala hauwafikii ukumbusho mpya kutoka kwa Arrahman ila wao hujitenga nao. [5]
Kwa yakini wamekanusha; kwa hivyo zitakuja wafikia khabari za yale waliyo kuwa wakiyafanyia mzaha. [6]
Je! Hawakuiona ardhi, mimea mingapi tumeiotesha humo, ya kila namna nzuri? [7]
Hakika katika haya zipo Ishara. Lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini. [8]
Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. [9]
Na Mola wako Mlezi, alipo mwita Musa, akamwambia: Fika kwa watu madhaalimu, [10]
Watu wa Firauni. Hawaogopi? [11]
Akasema: Hakika mimi nachelea wasinikanushe. [12]
Na kifua changu kina dhiki, na ulimi wangu haukunjuki vyema. Basi mtumie ujumbe Harun. [13]
Na wao wana kisasi juu yangu, kwa hivyo naogopa wasije kuniuwa. [14]
Akasema: Siyo hivyo kabisa! Nendeni na miujiza yetu. Hakika Sisi tu pamoja nanyi, tunasikiliza. [15]
Basi mfikieni Firauni na mwambieni: Hakika sisi ni Mitume wa Mola Mlezi wa walimwengu wote. [16]
Waachilie Wana wa Israili wende nasi. [17]
(Firauni) akasema: Sisi hatukukulea wewe utotoni, na ukakaa kwetu katika umri wako miaka mingi? [18]
Na ukatenda kitendo chako ulicho tenda, nawe ukawa miongoni mwa wasio na shukrani? [19]
(Musa) akasema: Nilitenda hayo hapo nilipo kuwa miongoni mwa wale walio potea. [20]
Basi nilikukimbieni nilipo kuogopeni, tena Mola wangu Mlezi, akanitunukia hukumu, na akanijaali niwe miongoni mwa Mitume. [21]
Na hiyo ndiyo neema ya kunisumbulia, na wewe umewatia utumwani Wana wa Israili? [22]
Firauni akasema: Na nani huyo Mola Mlezi wa walimwengu wote? [23]
Akasema: Ndiye Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, na viliomo baina yao, ikiwa nyinyi ni wenye yakini. [24]
(Firauni) akawaambia walio mzunguka: Hamsikilizi? [25]
(Musa) akasema: Ndiye Mola wenu Mlezi, na Mola Mlezi wa baba zenu wa kwanza. [26]
(Firauni) akasema: Hakika huyu Mtume wenu aliye tumwa kwenu ni mwendawazimu. [27]
. (Musa) akasema: Ndiye Mola Mlezi wa Mashariki na Magharibi na viliomo baina yao, ikiwa nyinyi mnatia akilini. [28]
(Firauni) akasema: Ukimfuata mungu mwengine asiye kuwa mimi, basi bila ya shaka nitakufunga gerezani. [29]
Akasema: Je! Ijapo kuwa nitakuletea kitu cha kubainisha wazi? [30]
Akasema: Kilete basi, kama wewe ni katika wasemao kweli. [31]
Basi akaitupa fimbo yake, mara ikawa nyoka wa kuonekana dhaahiri. [32]
Na akautoa mkono wake, na mara ukawa mweupe kwa watazamao. [33]
(Firauni) akawaambia waheshimiwa walio mzunguka: Hakika huyu ni mchawi mtaalamu. [34]
Anataka kukutoeni katika nchi yenu kwa uchawi wake. Basi mna shauri gani? [35]
Wakasema: Mpe muda yeye na nduguye na uwatume mijini wapigao mbiu ya mgambo. [36]
Wakuletee kila mchawi bingwa mtaalamu. [37]
Basi wakakusanywa wachawi wakati na siku maalumu. [38]
Na watu wakaambiwa: Je! Mtakusanyika? [39]
Huenda tutawafuata wachawi wakiwa wao ndio watakao shinda. [40]
Basi walipo kuja wachawi wakamwambia Firauni: Je! Tutapata ujira tukiwa sisi ndio tulio shinda? [41]
Naam! Na hakika mtakuwa katika watu wa mbele. [42]
Musa akwaambia: Tupeni mnavyo taka kutupa. [43]
Basi wakatupa kamba zao na fimbo zao, na wakasema: Kwa nguvu za Firauni hakika sisi hapana shaka ni wenye kushinda. [44]
Musa tena akatupa fimbo yake, nayo mara ikavimeza walivyo vizua. [45]
Hapo wachawi walipinduka wakasujudu. [46]
Wakasema: Tunamuamini Mola Mlezi wa walimwengu wote. [47]
Mola Mlezi wa Musa na Harun. [48]
(Firauni) akasema: Je! Mmemuamini kabla sijakuruhusuni? Bila ya shaka yeye basi ndiye mkubwa wenu aliye kufunzeni uchawi. Basi mtakuja jua! Nitakata mikono yenu na miguu yenu kwa kutafautisha. Na nitakubandikeni misalabani nyote. [49]
Wakasema: Haidhuru, kwani sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu Mlezi. [50]
Hakika sisi tunatumai Mola wetu Mlezi atatusamehe makosa yetu, kwa kuwa ndio wa kwanza wa kuamini. [51]
Na tulimuamrisha Musa kwa wahyi: Nenda na waja wangu wakati wa usiku. Kwa hakika mtafuatwa. [52]
Basi Firauni akawatuma mijini wapiga mbiu za mgambo. [53]
(Wakieneza): Hakika hawa ni kikundi kidogo. [54]
Nao wanatuudhi. [55]
Na sisi ni wengi, wenye kuchukua hadhari. [56]
Basi tukawatoa katika mabustani na chemchem, [57]
Na makhazina, na vyeo vya hishima, [58]
Kadhaalika; na tukawarithisha hayo Wana wa Israili. [59]
Basi wakawafuata lilipo chomoza jua. [60]
Na yalipo onana majeshi mawili haya, watu wa Musa wakasema: Hakika sisi bila ya shaka tumepatikana! [61]
(Musa) akasema: Hasha! Hakika yu pamoja nami Mola wangu Mlezi. Yeye ataniongoa! [62]
Tulimletea wahyi Musa tukamwambia: Piga bahari kwa fimbo yako. Basi ikatengana, na kila sehemu ikawa kama mlima mkubwa. [63]
Na tukawajongeza hapo wale wengine. [64]
Tukawaokoa Musa na walio kuwa pamoja naye wote. [65]
Kisha tukawazamisha hao wengine. [66]
Hakika bila ya shaka katika hayo ipo Ishara; lakini wengi wao si katika wenye kuamini. [67]
Na kwa hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. [68]
Na wasomee khabari za Ibrahim. [69]
Alipo mwambia baba yake na kaumu yake: Mnaabudu nini? [70]
Wakasema: Tunaabudu masanamu, daima tunayanyenyekea. [71]
Akasema: Je! Yanakusikieni mnapo yaita? [72]
Au yanakufaeni, au yanakudhuruni? [73]
Wakasema: Bali tumewakuta baba zetu wakifanya hivyo hivyo. [74]
Je! Mmewaona hawa mnao waabudu- [75]
Nyinyi na baba zenu wa zamani? [76]
Kwani hakika hao ni adui zangu, isipo kuwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. [77]
Ambaye ndiye aliye niumba, na Yeye ndiye ananiongoa, [78]
Na ambaye ndiye ananilisha na kuninywesha. [79]
Na ninapo ugua ni Yeye ndiye anaye niponesha. [80]
Na ambaye atanifisha, na kisha atanihuisha. [81]
Na ambaye ndiye ninaye mtumai kunisamehe makosa yangu Siku ya Malipo. [82]
Mola wangu Mlezi! Nitunukie hukumu na uniunganishe na watendao mema. [83]
Na unijaalie nitajwe kwa wema na watu watakao kuja baadaye. [84]
Na unijaalie katika warithi wa Bustani za neema. [85]
Na umsamehe baba yangu, kwani hakika alikuwa miongoni mwa wapotovu. [86]
Wala usinihizi Siku watapo fufuliwa. [87]
Siku ambayo kwamba mali hayato faa kitu wala wana. [88]
Isipo kuwa mwenye kumjia Mwenyezi Mungu na moyo safi. [89]
Na Pepo itasogezwa kwa wachamngu. [90]
Na Jahannamu itadhihirishwa kwa wapotovu. [91]
Na wataambiwa: Wako wapi mlio kuwa mkiwaabudu [92]
Badala ya Mwenyezi Mungu? Je! Wanakusaidieni, au wanajisaidia wenyewe? [93]
Basi watavurumizwa humo wao na hao wakosefu, [94]
Na majeshi ya Ibilisi yote. [95]
Watasema, na hali ya kuwa wanazozana humo: [96]
Wallahi! Kwa yakini tulikuwa katika upotovu ulio dhaahiri, [97]
Tulipo kufanyeni ni sawa na Mola Mlezi wa walimwengu wote. [98]
Tulipo kufanyeni ni sawa na Mola Mlezi wa walimwengu wote. [99]
Basi hatuna waombezi. [100]
Wala rafiki wa dhati. [101]
Laiti tungeli pata kurejea tena tungeli kuwa katika Waumini. [102]
Hakika katika haya ipo Ishara, lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini. [103]
Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. [104]
Kaumu ya Nuhu waliwakadhibisha Mitume. [105]
Alipo waambia ndugu yao, Nuhu: Je! Hamchimngu?. [106]
Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu. [107]
Basi Mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi. [108]
Na sikutakini juu yake ujira, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. [109]
Basi Mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi. [110]
Wakasema: Je! Tukuamini wewe, hali wanao kufuata ni watu wa chini?. [111]
Akasema: Nayajuaje waliyo kuwa wakiyafanya?. [112]
Hisabu yao haiko ila kwa Mola wao Mlezi, laiti mngeli tambua!. [113]
Wala mimi si wa kuwafukuza Waumini. [114]
Mimi si cho chote ila ni Mwonyaji wa dhaahiri shaahiri. [115]
Wakasema: Ikiwa huachi, ewe Nuhu, bila ya shaka utapigwa mawe. [116]
Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wamenikanusha. [117]
Basi hukumu baina yangu na wao kwa hukumu yako, na uniokoe mimi na walio pamoja nami, Waumini. [118]
Kwa hivyo tukamwokoa yeye na walio kuwa pamoja naye katika marikebu iliyo sheheni. [119]
Kisha tukawazamisha baadaye walio bakia. [120]
Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. [121]
Kina A'd waliwakanusha Mitume. [122]
Kina A'd waliwakanusha Mitume. [123]
Alipo waambia ndugu yao, Hud: Je! Hamchimngu? [124]
Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi. [125]
Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini. [126]
Wala sikutakeni juu yake ujira, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. [127]
Je! Mnajenga juu ya kila mnyanyuko kumbusho la kufanyia upuuzi? [128]
Na mnajenga majengo ya fakhari kama kwamba mtaishi milele! [129]
Na mnapo tumia nguvu mnatumia nguvu kwa ujabari. [130]
Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini. [131]
Na mcheni aliye kupeni haya mnayo yajua. [132]
Amekupeni wanyama wa kufuga na wana. [133]
Na mabustani na chemchem. [134]
Hakika mimi ninakukhofieni adhabu ya Siku Kubwa. [135]
Wakasema: Ni mamoja kwetu, ukitupa mawaidha au hukuwa miongoni mwa watoao mawaidha. [136]
Haya si chochote ila ni mtindo wa watu wa tokea zamani. [137]
Wala sisi hatutaadhibiwa. [138]
Wakamkanusha; nasi tukawaangamiza. Hakika bila ya shaka katika haya ipo Ishara. Lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini. [139]
Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. [140]
Kina Thamud waliwakanusha Mitume. [141]
Alipo waambia ndugu yao Swaleh: Je! Hamumchimngu? [142]
Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu. [143]
Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini. [144]
Wala sikutakini ujira juu yake. Ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. [145]
Je! Mtaachwa salama usalimina katika haya yaliyopo hapa? [146]
Katika mabustani, na chemchem? [147]
Na konde na mitende yenye makole yaliyo wiva. [148]
Na mnachonga milimani majumba kwa ustadi. [149]
Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi. [150]
Wala msit'ii amri za walio pindukia mipaka,. [151]
Ambao wanafanya ufisadi katika nchi, wala hawatengenezi. [152]
Wakasema: Hakika wewe ni miongoni mwa walio rogwa. [153]
Wewe si chochote ila ni mtu kama sisi. Basi lete Ishara ukiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli. [154]
Akasema: Huyu ngamia jike; awe na zamu yake ya kunywa, na nyinyi muwe na zamu yenu ya kunywa katika siku maalumu. [155]
Wala ms!imguse kwa uwovu, isije ikakushikeni adhabu ya Siku Kubwa. [156]
Lakini wakamuuwa, na wakawa wenye kujuta. [157]
Basi ikawapata adhabu. Hakika katika hayo ipo Ishara. Lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini. [158]
Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. [159]
Watu wa Luut'i waliwakanusha Mitume. [160]
Alipo waambia ndugu yao, Luut'i: Je! Hamumchimngu?. [161]
Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu kwenu. [162]
Basi mcheni Mwenyezi Mungu na nit'iini mimi. [163]
Wala mimi sikutakini ujira juu yake; ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. [164]
Je! Katika viumbe vyote mnawaingilia wanaume?. [165]
Na mnaacha alicho kuumbieni Mola wenu Mlezi katika wake zenu? Ama kweli nyinyi ni watu mnao ruka mipaka!. [166]
Wakasema: Ewe Luut'i! Usipo acha, hapana shaka utakuwa miongoni mwa wanao tolewa mji!. [167]
Akasema: Hakika mimi ni katika wanao kichukia hichi kitendo chenu. [168]
Mola wangu Mlezi! Niokoe mimi na ahali zangu na haya wayatendayo. [169]
Basi tukamwokoa yeye na ahali zake wote,. [170]
Isipo kuwa kikongwe katika walio kaa nyuma. [171]
Kisha tukawaangamiza wale wengine. [172]
Na tukawanyeshea mvua, basi ni ovu mno mvua ya waliyo onywa. [173]
Hakika katika hayo ipo Ishara. Na hawakuwa wengi wao wenye kuamini. [174]
Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu. [175]
Watu wa Machakani waliwakanusha Mitume. [176]
Shuaibu alipo waambia: Je! Hamfanyi mkamchamngu?. [177]
Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu. [178]
Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi. [179]
Wala sikutakini ujira juu yake. Ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. [180]
Timizeni kipimo sawa sawa, wala msiwe katika wanao punja. [181]
Na pimeni kwa haki iliyo nyooka;. [182]
Wala msiwapunje watu vitu vyao, wala msifanye jeuri kwa ufisadi. [183]
Na mcheni aliye kuumbeni nyinyi na vizazi vilivyo tangulia. [184]
Wakasema: Hakika wewe ni katika walio rogwa. [185]
Na wewe si chochote ila ni mtu tu kama sisi, na kwa yakini tunakuona wewe ni katika waongo. [186]
Hebu tuangushie vipande kutoka mbinguni ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli. [187]
Akasema: Mola wangu Mlezi anajua zaidi mnayo yatenda. [188]
Basi walimkanusha, na ikawashika adhabu ya siku ya kivuli. Hakika hiyo ilikuwa adhabu ya siku kubwa. [189]
Hakika katika hayo ipo Ishara, lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini. [190]
Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. [191]
Na bila ya shaka hii ni Uteremsho wa Mola Mlezi wa walimwengu wote. [192]
Ameuteremsha Roho muaminifu,. [193]
Juu ya moyo wako, ili uwe katika Waonyaji,. [194]
Kwa ulimi wa Kiarabu ulio wazi. [195]
Na hakika bila ya shaka haya yamo katika Vitabu vya kale. [196]
Je! Haikuwa kwao ni Ishara kwamba wanayajua haya wanazuoni wa Wana wa Israili?. [197]
Na lau kuwa tungeli iteremsha juu ya mmoja wa wasio kuwa Waarabu,. [198]
Na akawasomea, wasingeli kuwa wenye kuamini. [199]
Namna hivi tunaingiza katika nyoyo za wakosefu. [200]
Hawataiamini mpaka waione adhabu chungu. [201]
Basi itawafikia kwa ghafla, na hali hawana khabari. [202]
Na watasema: Je, tutapewa muhula?. [203]
Basi, je, wanaihimiza adhabu yetu?. [204]
Waonaje kama tukiwastarehesha kwa miaka,. [205]
Kisha yakawafikia waliyo kuwa wakiahidiwa,. [206]
Yatawafaa nini yale waliyo stareheshewa?. [207]
Wala hatukuangamiza mji wo wote ila ulikuwa na waonyaji. [208]
Kuwa ni ukumbusho. Wala Sisi hatukuwa wenye kudhulumu. [209]
Wala Mashet'ani hawakuteremka nayo, [210]
Wala haitakiwi kwao, na wala hawawezi. [211]
Hakika hao wametengwa na kusikia. [212]
Basi usimwombe mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu ukawa miongoni mwa watakao adhibiwa. [213]
Na uwaonye jamaa zako walio karibu nawe. [214]
Na watwae kwa upole wanao kufuata miongoni mwa Waumini. [215]
Na ikiwa watakuasi basi sema: Mimi najitenga mbali na hayo mnayo yatenda. [216]
Na umtegemee Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. [217]
Ambaye anakuona unapo simama, [218]
Na mageuko yako kati ya wanao sujudu. [219]
Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua. [220]
Je! Nikwambieni nani wanawashukia Mashet'ani? [221]
Wanamshukia kila mzushi mkubwa mwingi wa dhambi. [222]
Wanawapelekea yale wanayo yasikia; na wengi wao ni waongo. [223]
Na watungaji mashairi ni wapotofu ndio wanawafuata. [224]
Je! Huwaoni kwamba wao wanatangatanga katika kila bonde? [225]
Na kwamba wao husema wasiyo yatenda? [226]
Isipo kuwa wale walio amini, na wakatenda mema, na wakamkumbuka Mwenyezi Mungu kwa wingi, na wakajitetea wanapo dhulumiwa. Na wanao dhulumu watakuja jua mgeuko gani watakao geuka. [227]