The Noble Qur'an Encyclopedia
Towards providing reliable exegeses and translations of the meanings of the Noble Qur'an in the world languagesYa Seen [Ya Seen] - Swahili translation - Ali Muhsen Al-Berwani
Surah Ya Seen [Ya Seen] Ayah 83 Location Maccah Number 36
Ya-Sin (Y.S.). [1]
Kwa Haki ya Qur'ani yenye hikima! [2]
Hakika wewe ni miongoni mwa walio tumwa! [3]
Juu ya Njia Iliyo Nyooka. [4]
Uteremsho wa Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu. [5]
Ili uwaonye watu ambao baba zao hawakuonywa , basi wao wamekuwa wenye kughafilika. [6]
Bila ya shaka kauli imekwisha thibiti juu ya wengi katika wao, kwa hivyo hawaamini. [7]
Tumeweka makongwa shingoni mwao, yakawafika videvuni. Kwa hivyo vichwa vyao viko juu tu. [8]
Tumeweka kizuizi mbele yao, na kizuizi nyuma yao, na tumewafunika macho yao; kwa hivyo hawaoni. [9]
Ni sawa sawa kwao ukiwaonya au usiwaonye, hawataamini. [10]
Hakika wewe unamwonya mwenye kufuata ukumbusho, na akamcha Arrahman, Mwingi wa Rehema, kwa ghaibu. Basi mbashirie huyo msamaha na ujira mwema. [11]
Hakika Sisi tunawafufua wafu, na tunayaandika wanayo yatanguliza, na wanayo yaacha nyuma. Na kila kitu tumekihifadhi katika daftari asli lenye kubainisha. [12]
Na wapigie mfano wa wakaazi wa mji walipo wafikia walio tumwa. [13]
Tulipo watumia wawili, wakawakanusha. Basi tukawazidishia nguvu kwa mwingine wa tatu. Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwenu. [14]
Wakasema: Nyinyi si chochote ila ni watu kama sisi. Na Mwingi wa Rehema hakuteremsha kitu. Nyinyi mnasema uwongo tu. [15]
Wakasema: Mola wetu Mlezi anajua kwamba hakika sisi tumetumwa kwenu. [16]
Wala si juu yetu ila kufikisha ujumbe ulio wazi. [17]
Wakasema: Sisi tumeagua kuwa nyinyi ni wakorofi. Ikiwa hamtaacha basi kwa yakini tutakupigeni mawe, na mtapata adhabu chungu kutoka kwetu. [18]
Wakasema: Ukorofi wenu mnao wenyewe! Je! Ni kwa kuwa mnakumbushwa? Ama nyinyi ni watu walio pindukia mipaka. [19]
Na akaja mtu mbio kutokea upande wa mbali wa mjini, akasema: Enyi watu wangu! Wafuateni hawa walio tumwa. [20]
Wafuateni ambao hawakutakini ujira, hali ya kuwa wenyewe wameongoka. [21]
NA KWA NINI nisimuabudu yule aliye niumba na kwake mtarejeshwa? [22]
Je! Niishike miungu mingine badala yake? Arrahmani, Mwingi wa Rehema, akinitakia madhara uombezi wa hao hautanifaa kitu, wala hawataniokoa. [23]
Basi hakika mimi hapo nitakuwa katika upotovu ulio dhaahiri. [24]
Hakika mimi nimemuamini Mola wenu Mlezi, basi nisikilizeni! [25]
Akaambiwa: Ingia Peponi! Akasema: Laiti kuwa watu wangu wangeli jua [26]
Jinsi Mola wangu Mlezi alivyo nisamehe, na akanifanya miongoni mwa walio hishimiwa. [27]
Na hatukuwateremshia kaumu yake baada yake jeshi kutoka mbinguni, wala si wenye kuteremsha. [28]
Hakukuwa ila ukelele mmoja tu; na mara walizimwa! [29]
Nawasikitikia waja wangu. Hawajii Mtume ila wao humkejeli. [30]
Je! Hawaoni umma ngapi tulizo ziangamiza kabla yao? Hakika hao hawarejei tena kwao. [31]
Na hapana mmoja ila wote watakusanywa waletwe mbele yetu. [32]
Na Ishara hiyo kwao - ardhi iliyo kufa, nasi tukaifufua, na tukatoa ndani yake nafaka, wakawa wanazila! [33]
Na tukafanya ndani yake mabustani ya mitende na mizabibu, na tukatimbua chemchem ndani yake, [34]
Ili wale matunda yake, na hayo hayakufanywa na mikono yao! Basi je, hawashukuru? [35]
Subhana, Ametakasika, aliye umba dume na jike vyote katika vinavyo mea katika ardhi na katika nafsi zao, na katika wasivyo vijua. [36]
Na usiku ni Ishara kwao. Tunauvua humo mchana, mara wao wanakuwa gizani. [37]
Na jua linakwenda kwa kiwango chake. Hayo ni makadirio ya Mwenye nguvu, Mwenye kujua. [38]
Na mwezi tumeupimia vituo, mpaka unakuwa kama karara kongwe. [39]
Haliwi jua kuufikia mwezi, wala usiku kuupita mchana. Na vyote vinaogelea katika njia zao. [40]
Na ni Ishara kwao kwamba Sisi tuliwapakia dhuriya zao katika jahazi ilio sheheni. [41]
Na tukawaumbia kutoka mfano wake wanavyo vipanda. [42]
Na tukitaka tunawazamisha, wala hapana wa kuwasaidia, wala hawaokolewi, [43]
Isipo kuwa kwa rehema zitokazo kwetu na starehe kwa muda. [44]
Na wanapo ambiwa: Jilindeni na yalioko mbele yenu na yalioko nyuma yenu, ili mpate kurehemewa [45]
Na haiwafikii Ishara yoyote katika Ishara za Mola wao Mlezi ila wao huwa ni wenye kuipuuza. [46]
Na wanapo ambiwa: Toeni katika aliyo kupeni Mwenyezi Mungu, walio kufuru huwaambia walio amini: Je! Tuwalishe ambao Mwenyezi Mungu angependa angeli walisha mwenyewe? Nyinyi hammo ila katika upotofu ulio dhaahiri. [47]
Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi ni wakweli? [48]
Hawangojei ila ukelele mmoja tu utakao wachukua nao wamo kuzozana. [49]
Basi hawataweza kuusia, wala kwa watu wao hawarejei. [50]
Na litapulizwa barugumu, mara watatoka makaburini wakikimbilia kwa Mola wao Mlezi. [51]
Watasema: Ole wetu! Nani aliye tufufua kwenye malazi yetu? Haya ndiyo aliyo yaahidi Mwingi wa Rehema na wakasema kweli Mitume. [52]
Haitakuwa ila ukelele mmoja tu, mara wote watahudhuruishwa mbele yetu. [53]
Basi leo nafsi yoyote haitadhulumiwa kitu, wala hamtalipwa ila yale mliyo kuwa mkiyatenda. [54]
Hakika watu wa Peponi leo wamo shughulini, wamefurahi. [55]
Wao na wake zao wamo katika vivuli wameegemea juu ya viti vya fakhari. [56]
Watapata humo kila namna ya matunda na watapata kila watakacho kitaka. [57]
"Salama!" Hiyo ndiyo kauli itokayo kwa Mola Mlezi Mwenye kurehemu. [58]
Na enyi wakosefu! Jitengeni leo! [59]
Je! Sikuagana nanyi, enyi wanaadamu, kuwa msimuabudu Shet'ani? Hakika yeye ni adui dhaahiri kwenu. [60]
Na ya kwamba mniabudu Mimi? Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka. [61]
Na bila ya shaka yeye amekwisha lipoteza kundi kubwa miongoni mwenu. Je, hamkuwa mkifikiri? [62]
Hii basi ndiyo Jahannamu mliyo kuwa mkiahidiwa. [63]
Ingieni leo kwa vile mlivyo kuwa mkikufuru. [64]
Leo tunaviziba vinywa vyao, na iseme nasi mikono yao, na itoe ushahidi miguu yao kwa waliyo kuwa wakiyachuma. [65]
Na tungeli penda tungeli yafutilia mbali macho yao, wakawa wanaiwania njia. Lakini wange ionaje? [66]
Na tungeli taka tunge wageuza sura hapo hapo walipo, basi wasinge weza kwenda wala kurudi. [67]
Na tunaye mzeesha tunamrudisha nyuma katika umbo. Basi je! hawazingatii? [68]
Wala hatukumfundisha (Muhammad) mashairi, wala hayatakikani kwake hayo. Haukuwa huu ila ni ukumbusho na Qur'ani inayo bainisha. [69]
Ili imwonye aliye hai, na neno litimie juu ya makafiri. [70]
Je! Hawaoni kwamba tumewaumbia kutokana na iliyo fanya mikono yetu wanyama wa mifugo, na wao wakawa wenye kuwamiliki. [71]
Na Sisi tukawadhalilishia. Basi baadhi yao wako wanao wapanda, na baadhi yao wanawala. [72]
Na wao wanapata kwao manufaa na vinywaji. Basi je, hawashukuru? [73]
Na wameishika miungu mingine badala ya Mwenyezi Mungu ili ati wapate kusaidiwa! [74]
Hawataweza kuwasaidia. Bali hao ndio watakuwa askari wao watakao hudhurishwa. [75]
Basi maneno yao yasikuhuzunishe. Hakika Sisi tunayajua wanayo yaweka siri na wanayo yatangaza. [76]
Kwani mwanaadamu haoni ya kwamba Sisi tumemuumba yeye kutokana na tone la manii? Kisha sasa yeye ndio amekuwa ndiye mgomvi wa dhaahiri! [77]
Na akatupigia mfano, na akasahau kuumbwa kwake, akasema: Ni nani huyo atakaye ihuisha mifupa nayo imekwisha mung'unyika? [78]
Sema: Ataihuisha huyo huyo aliye iumba hapo mara ya mwanzo. Na Yeye ni Mjuzi wa kila kuumba. [79]
Aliye kujaalieni kupata moto kutokana na mti wa kijani nanyi mkawa kwa huo mnawasha. [80]
Kwani aliye ziumba mbingu na ardhi hawezi kuwaumba mfano wao? Kwani! Naye ndiye Muumbaji Mkuu, Mjuzi. [81]
Hakika amri yake anapo taka kitu ni kukiambia tu: Kuwa! Na kikawa. [82]
Basi Ametakasika yule ambaye mkononi mwake umo Ufalme wa kila kitu; na kwake Yeye mtarejeshwa. [83]