The Noble Qur'an Encyclopedia
Towards providing reliable exegeses and translations of the meanings of the Noble Qur'an in the world languagesOrnaments of Gold [Az-Zukhruf] - Swahili translation - Ali Muhsen Al-Berwani
Surah Ornaments of Gold [Az-Zukhruf] Ayah 89 Location Maccah Number 43
H'a Mim . [1]
Naapa kwa Kitabu kinacho bainisha. [2]
Hakika Sisi tumeifanya Qur'ani kwa Kiarabu ili mfahamu. [3]
Na hakika hiyo imo katika Asili ya Maandiko yalioko kwetu, ni tukufu na yenye hikima. [4]
Je! Tuache kukukumbusheni kabisa kwa kuwa nyinyi ni watu mlio pita mipaka kwa ukafiri? [5]
Na Manabii wangapi tuliwatuma kwa watu wa zamani! [6]
Na hawajii Nabii yeyote ila walikuwa wakimkejeli. [7]
Na tuliwaangamiza walio kuwa na nguvu kushinda wao. Na mfano wa watu wa zamani umekwisha pita. [8]
Na ukiwauliza: Nani aliye ziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka watasema: Kaziumba Mwenye nguvu, Mjuzi! [9]
ٱلَّذِي جَعَلَ لَكُمُ ٱلۡأَرۡضَ مَهۡدٗا وَجَعَلَ لَكُمۡ فِيهَا سُبُلٗا لَّعَلَّكُمۡ تَهۡتَدُونَ [١٠]
Ambaye amekufanyieni ardhi kama tandiko, na akakufanyieni ndani yake njia mpate kuongoka. [10]
Na ambaye ndiye aliye teremsha kutoka mbinguni maji kwa kiasi, na kwa hayo tukaifufua nchi iliyo kufa. Na namna hivi ndivyo mtakavyo tolewa. [11]
Na ambaye ndiye aliye umba katika kila kitu jike na dume, na akakufanyieni marikebu na wanyama mnao wapanda. [12]
Ili mkae vizuri migongoni mwao, kisha mkumbuke neema za Mola wenu Mlezi mnapokaa sawa sawa juu yao na mseme: Ametakasika aliye mfanya huyu atutumikie, na tusingeli weza kufanya haya wenyewe. [13]
Na hakika sisi tutarudi kwa Mola wetu Mlezi. [14]
Na wanamfanyia katika waja wake fungu. Kwa hakika mwanaadamu ni mtovu wa fadhila aliye dhaahiri. [15]
Au amejichukulia watoto wanawake katika vile alivyo viumba, na akakuteulieni nyinyi watoto wanaume? [16]
Na anapo bashiriwa mmoja wao kwa yale aliyo mpigia mfano Mwenyezi Mungu, uso wake husawijika na hujaa hasira. [17]
Ati aliye lelewa katika mapambo, na katika mabishano hawezi kusema kwa bayana? [18]
Na wakawafanya Malaika, ambao ni waja wa Mwingi wa Rehema, ni wanawake! Kwani wameshuhudia kuumbwa kwao? Ushahidi wao utaandikwa na wao watahojiwa! [19]
Nao husema: Angeli penda Mwingi wa Rehema tusingeli waabudu sisi. Hawana ujuzi wowote wa hayo! Hawana ila kusema uwongo tu! [20]
Kwani tuliwapa Kitabu kabla ya hichi, na ikawa wao wanakishikilia hicho? [21]
Bali wanasema: Hakika sisi tuliwakuta baba zetu wanashika dini makhsusi, basi na sisi tunaongoza nyayo zao. [22]
Na kadhaalika hatukumtuma mwonyaji kwenye mji wowote ila watu wake walio deka kwa starehe walisema: Hakika sisi tuliwakuta baba zetu wanashika dini makhsusi, na sisi tunafuata nyayo zao. [23]
Akasema (Mwonyaji): Hata nikikuleteeni yenye uwongofu bora kuliko mlio wakuta nao baba zenu? Wakasema: Sisi tunayakataa tu hayo mliyo tumwa. [24]
Basi tukawalipizia. Angalia ulikuwaje mwisho wa walio kadhibisha! [25]
Na pale Ibrahim alipo mwambia baba yake na kaumu yake: Hakika mimi ninajitenga mbali na hayo mnayo yaabudu, [26]
Isipo kuwa yule aliye niumba, kwani Yeye ataniongoa. [27]
Na akalifanya hili liwe neno lenye kubaki katika vizazi vyake ili warejee. [28]
Bali tuliwastarehesha hawa na baba zao mpaka ikawafikia Haki na Mtume aliye bainisha. [29]
Na ilipo wafikia Haki wakasema: Huu ni uchawi, na sisi hakika tunaukataa. [30]
Na walisema: Kwa nini Qur'ani hii haikuteremshwa kwa mtu mkubwa katika miji miwili hii? [31]
Kwani wao ndio wanao gawa rehema za Mola wako Mlezi? Sisi tumewagawanyia baina yao maisha yao katika uhai wa duniani, na tukawanyanyua baadhi yao juu ya wengine kwa daraja nyingi; kwa hivyo baadhi yao wanawafanya wenginewe wawatumikie. Na rehema za Mwenyezi Mungu ni bora kuliko hayo wanayo yakusanya. [32]
Na lau isinge kuwa watu watakuwa kundi moja tungeli wajaalia wanao mkufuru Rahmani wana nyumba zao zina dari ya fedha, na ngazi zao pia wanazo pandia, [33]
Na milango ya nyumba zao na vitanda wanavyo egemea juu yake, [34]
Na mapambo. Lakini hayo si chochote ila ni starehe ya maisha ya dunia tu, na Akhera iliyoko kwa Mola wako Mlezi ni ya wenye kumchamngu. [35]
Anaye yafanyia upofu maneno ya Rahmani tunamwekea Shet'ani kuwa ndiye rafiki yake. [36]
Na hakika wao wanawazuilia Njia na wenyewe wanadhani kuwa wameongoka. [37]
Hata atakapo tujia atasema: Laiti ungeli kuwako baina yangu na wewe kama umbali baina ya mashariki na magharibi. Rafiki mwovu mno wewe! [38]
Na kwa kuwa mlidhulumu, haitakufaeni kitu leo kwamba nyinyi mnashirikiana katika adhabu. [39]
Je! Unaweza kuwasikilizisha viziwi, au unaweza kuwaongoa vipofu na waliomo katika upotofu ulio wazi? [40]
Na hata tukikuondoa, Sisi tutalipiza kisasi chetu kwao. [41]
Au tutakuonyesha tulio waahidi. Nasi bila ya shaka tuna uweza juu yao. [42]
Basi wewe yashike yaliyo funuliwa kwako. Hakika wewe uko kwenye Njia Iliyo Nyooka. [43]
Na hakika haya ni ukumbusho kwako na kwa kaumu yako. Na mtakuja ulizwa. [44]
Na waulize Mitume wetu tulio watuma kabla yako: Je! Tulifanya miungu mingine iabudiwe badala ya Rah'mani? [45]
Na bila ya shaka tulimtuma Musa kwa Ishara zetu ende kwa Firauni na waheshimiwa wake, na akasema: Hakika mimi ni Mtume wa Mola Mlezi wa walimwengu wote! [46]
Lakini alipo wajia na Ishara zetu wakaingia kuzicheka. [47]
Na hatukuwaonyesha Ishara yoyote ila hiyo ilikuwa kubwa zaidi kuliko nyenginewe. Na tukawakamata kwa adhabu ili warejee. [48]
Na wakasema: Ewe mchawi! Tuombee kwa Mola wako Mlezi kwa ile ahadi aliyo kuahidi; hakika sisi tutakuwa wenye kuongoka. [49]
Basi tulipo waondolea adhabu hiyo, mara wakaingia kuvunja ahadi. [50]
Na Firauni alitangaza kwa watu wake, akisema: Enyi watu wangu! Kwani mimi sinao huu ufalme wa Misri, na hii mito inapita chini yangu? Je! Hamwoni? [51]
Au mimi si bora kuliko huyu aliye mnyonge, wala hawezi kusema waziwazi? [52]
Basi mbona hakuvikwa vikuku vya dhahabu, au hawakuja Malaika pamoja naye wakamwandama? [53]
Basi aliwachezea watu wake, na wakamt'ii. Kwa hakika hao walikuwa watu wapotovu. [54]
Walipo tukasirisha tuliwapatiliza tukawazamisha wote! [55]
Walipo tukasirisha tuliwapatiliza tukawazamisha wote! [56]
Na alipo pigiwa mfano Mwana wa Mariamu, watu wako waliupiga ukelele. [57]
Wakasema: Miungu yetu kwani si bora kuliko huyu? Hawakukupigia mfano huo ila kwa ubishi tu. Bali hao ni watu wagomvi! [58]
Hakuwa yeye (Isa) ila ni Mtumwa tuliye mneemesha na tukamfanya ni mfano kwa Wana wa Israili. [59]
Na tungeli penda tungeli wafanyia miongoni mwenu Malaika katika ardhi wakifuatana. [60]
Na kwa hakika yeye ni alama ya Saa ya Kiyama. Basi usiitilie shaka, na nifuateni. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka. [61]
Wala asikuzuilieni Shet'ani. Hakika yeye ni adui yenu wa dhaahiri. [62]
Na alipo kuja Isa na dalili zilizo wazi, alisema: Nimekujieni na hikima, na ili nikuelezeni baadhi ya yale mliyo khitalifiana. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na mnit'ii mimi. [63]
Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi, na ni Mola wenu Mlezi. Basi Muabuduni Yeye tu. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka. [64]
Lakini makundi kwa makundi yao yalikhitalifiana wao kwa wao. Ole wao walio dhulumu kwa adhabu ya siku chungu. [65]
Je! Nini wanangojea ila Saa iwajie kwa ghafla na wala wao hawatambui? [66]
Siku hiyo marafiki watakuwa ni maadui, wao kwa wao, isipo kuwa wachamngu. [67]
Enyi waja wangu! Hamtakuwa na khofu siku hiyo, wala hamtahuzunika. [68]
Ambao waliziamini Ishara zangu na walikuwa Waislamu. [69]
Ingieni Peponi, nyinyi na wake zenu; mtafurahishwa humo. [70]
Watakuwa wanapitishiwa sahani za dhahabu na vikombe; na vitakuwamo ambavyo nafsi zinavipenda na macho yanavifurahia, na nyinyi mtakaa humo milele. [71]
Na hiyo ni Pepo mliyo rithishwa kwa hayo mliyo kuwa mkiyafanya. [72]
Mnayo humo matunda mengi mtakayo yala. [73]
Kwa hakika wakosefu watakaa katika adhabu ya Jahannamu. [74]
Hawatapumzishwa nayo na humo watakata tamaa. [75]
Wala Sisi hatukuwadhulumu, bali wao ndio walio kuwa madhaalimu. [76]
Nao watapiga kelele waseme: Ewe Malik! Na atufishe Mola wako Mlezi! Naye aseme: Hakika nyinyi mtakaa humo humo! [77]
Kwa yakini tulikuleteeni Haki, lakini wengi katika nyinyi mlikuwa mnaichukia Haki. [78]
Au waliweza kupitisha amri yao? Bali ni Sisi ndio tunao pitisha. [79]
Au wanadhani kwamba hatusikii siri zao na minong'ono yao? Wapi! Na wajumbe wetu wapo karibu nao, wanayaandika. [80]
Sema: Ingeli kuwa Rahmani ana mwana, basi mimi ningeli kuwa wa kwanza kumuabudu. [81]
Ametakasika Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, Mola Mlezi wa A'rshi, na hayo wanayo msifia. [82]
Basi waache wapige porojo wakicheza mpaka wakutwe na hiyo siku yao waliyo ahidiwa. [83]
Na Yeye ndiye Mungu mbinguni, na ndiye Mungu katika ardhi. Naye ndiye Mwenye hikima, Mwenye ujuzi. [84]
Na ametukuka Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi na viliomo ndani yake. Na uko kwake ujuzi wa Saa ya Kiyama, na kwake Yeye mtarudishwa. [85]
Wala hao mnao waomba badala yake Yeye hawana uweza wa kumwombea mtu, isipo kuwa anaye shuhudia kwa haki, na wao wanajua. [86]
Na ukiwauliza ni nani aliye waumba? Bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu! Basi ni wapi wanako geuziwa? [87]
Na usemi wake (Mtume) ni: Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika hawa ni watu wasio amini. [88]
Basi wasamehe, na uwambie maneno ya salama. Watakuja jua. [89]