The Noble Qur'an Encyclopedia
Towards providing reliable exegeses and translations of the meanings of the Noble Qur'an in the world languagesThe Smoke [Ad-Dukhan] - Swahili translation - Ali Muhsen Al-Berwani
Surah The Smoke [Ad-Dukhan] Ayah 59 Location Maccah Number 44
H'a Mim . [1]
Naapa kwa Kitabu kinacho bainisha! [2]
Hakika tumekiteremsha katika usiku ulio barikiwa. Hakika Sisi ni Waonyaji. [3]
Katika usiku huu hubainishwa kila jambo la hikima! [4]
Jambo litokalo kwetu. Hakika Sisi ndio wenye kutuma. [5]
Ni rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia Mwenye kujua. [6]
Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na vilio baina yao, ikiwa nyinyi mna yakini. [7]
Hakuna mungu ila Yeye; anahuisha na anafisha- Mola Mlezi wenu na Mola Mlezi wa baba zenu wa mwanzo. [8]
Lakini wao wanacheza katika shaka. [9]
Basi ingoje siku ambayo mbingu zitakapo leta moshi ulio dhaahiri, [10]
Utakao wafunika watu: Hii ni adhabu chungu! [11]
Mola wetu Mlezi! Tuondolee adhabu hii. Hakika tutaamini. [12]
Nini faida ya kukumbuka kwao? Na alikwisha wafikia Mtume mwenye kubainisha. [13]
Na wao wakamgeuzia uso, na wakasema: Huyu amefunzwa, naye ni mwendawazimu. [14]
Hakika sisi tutaiondoa adhabu kidogo, lakini nyinyi kwa yakini mtarejea vile vile! [15]
Siku tutayo yashambulia mashambulio makubwa, bila ya shaka Sisi ni wenye kutesa. [16]
Na hakika kabla ya hawa tuliwafanyia mtihani watu wa Firauni, na aliwafikia Mtume Mtukufu. [17]
Akasema: Nipeni waja wa Mwenyezi Mungu; kwa hakika mimi kwenu ni Mtume Muaminifu. [18]
Na msimfanyie kiburi Mwenyezi Mungu; hakika mimi nitakuleteeni uthibitisho ulio wazi. [19]
Nami najikinga kwa Mola wangu Mlezi na ndiye Mola wenu Mlezi pia, ili msinipige mawe. [20]
Na ikiwa hamniamini, basi jitengeni nami. [21]
Ndipo akamwomba Mola wake Mlezi: Hakika watu hawa ni wakosefu. [22]
Mwenyezi Mungu akasema: Basi nenda na waja wangu usiku. Kwa yakini mtafuatwa. [23]
Na iache bahari vivyo hivyo imeachana, hakika wao hao ni jeshi litakalo zamishwa. [24]
Mabustani mangapi, na chemchem ngapi waliziacha! [25]
Na mimea na vyeo vitukufu! [26]
Na neema walizo kuwa wakijistareheshea! [27]
Ndio hivyo! Na tukawarithisha haya watu wenginewe. [28]
La mbingu wala ardhi hazikuwalilia, wala hawakupewa muhula. [29]
Na bila ya shaka tuliwaokoa Wana wa Israili katika adhabu ya kuwadhalilisha, [30]
Ya Firauni. Hakika yeye alikuwa jeuri katika wenye kupindukia mipaka. [31]
Na tuliwakhiari kwa ujuzi wetu kuliko walimwengu wenginewe. [32]
Na tukawapa katika ishara zenye majaribio yaliyo wazi. [33]
Hakika hawa wanasema: [34]
Hapana ila kufa kwetu mara ya kwanza tu, wala sisi hatufufuliwi. [35]
Basi warudisheni baba zetu, ikiwa nyinyi mnasema kweli. [36]
Je! Ni wao bora au watu wa Tubbaa' na walio kuwa kabla yao? Tuliwaangamiza. Hakika hao walikuwa wakosefu. [37]
Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake kwa mchezo. [38]
Hatukuviumba hivyo ila kwa Haki, lakini wengi wao hawajui. [39]
Hakika siku ya Uamuzi ni wakati ulio wekwa kwa wao wote. [40]
Siku ambayo rafiki hatamfaa rafiki yake kwa chochote, wala hawatanusuriwa. [41]
Isipo kuwa atakaye mrehemu Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu. [42]
Hakika Mti wa Zaqqum, [43]
Ni chakula cha mwenye dhambi. [44]
Kama shaba iliyo yayushwa, hutokota matumboni [45]
Kama kutokota kwa maji ya moto. [46]
(Itasemwa:) Mkamateni na mtupeni katikati ya Jahannamu! [47]
Kisha mmwagieni juu ya kichwa chake adhabu ya maji yanayo chemka. [48]
Onja! Ati wewe ndiye mwenye nguvu, mtukufu! [49]
Hakika haya ndiyo mliyo kuwa mkiyatilia shaka. [50]
Hakika wachamngu watakuwa katika mahali pa amani, [51]
Katika mabustani na chemchem, [52]
Watavaa hariri nyepesi na hariri nzito wakikabiliana, [53]
Hivi ndivyo itakavyo kuwa, na tutawaoza mahurilaini. [54]
Humo watataka kila aina ya matunda, na wakae kwa amani. [55]
Humo hawataonja mauti ila mauti yale ya kwanza, na (Mwenyezi Mungu) atawalinda na adhabu ya Jahannamu, [56]
Kuwa ni fadhila zitokazo kwa Mola wako Mlezi. Huko ndiko kufuzu kukubwa. [57]
Basi tumeifanya nyepesi hii Qur'ani kwa ulimi wako, ili wapate kukumbuka. [58]
Ngoja tu, na wao wangoje pia. [59]