The Noble Qur'an Encyclopedia
Towards providing reliable exegeses and translations of the meanings of the Noble Qur'an in the world languagesQaf [Qaf] - Swahili translation - Ali Muhsen Al-Berwani
Surah Qaf [Qaf] Ayah 45 Location Maccah Number 50
Qaaf. Naapa kwa Qur'ani tukufu! [1]
Bali wanastaajabu kwamba amewafikia mwonyaji kutoka miongoni mwao, na wakasema makafiri: Hili ni jambo la ajabu! [2]
Ati tukifa na tukawa udongo? Kurejea huko kuko mbali! [3]
Hakika Sisi tunajua kiasi cha kila kinacho punguzwa na ardhi kutokana nao. Na kwetu kipo Kitabu kinacho hifadhi yote. [4]
Lakini waliikanusha Haki ilipo wajia; kwa hivyo wamo katika mambo ya mkorogo. [5]
Je! Hawaangalii mbingu zilizo juu yao! Vipi tulivyo zijenga, na tukazipamba. Wala hazina nyufa. [6]
Na ardhi tumeitandaza na tukaiwekea milima, na tukaiotesha mimea mizuri ya kila namna. [7]
Yawe haya ni kifumbua macho na ukumbusho kwa kila mja mwenye kuelekea. [8]
وَنَزَّلۡنَا مِنَ ٱلسَّمَآءِ مَآءٗ مُّبَٰرَكٗا فَأَنۢبَتۡنَا بِهِۦ جَنَّٰتٖ وَحَبَّ ٱلۡحَصِيدِ [٩]
Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji yaliyo barikiwa, na kwa hayo tukaotesha mabustani na nafaka za kuvunwa. [9]
Na mitende mirefu yenye makole yaliyo zaa kwa wingi, [10]
Ili iwe ni riziki kwa waja wangu. Na tukaifufua kwa maji nchi iliyo kuwa imekufa. Kama hivyo ndivyo utakavyo kuwa ufufuaji. [11]
Kabla yao walikadhibisha kaumu ya Nuhu na wakaazi wa Rassi na Thamudi. [12]
Na A'di na Firauni na kaumu ya Lut'i. [13]
Na wakaazi wa Machakani, na watu wa Tubbaa'. Wote hao waliwakanusha Mitume, kwa hivyo onyo likathibitika juu yao. [14]
Kwani tulichoka kwa kuumba mara ya kwanza. Bali wao wamo katika shaka tu juu ya umbo jipya. [15]
Na hakika tumemuumba mtu, nasi tunayajua yanayo mpitikia katika nafsi yake. Na Sisi tuko karibu naye kuliko mshipa wa shingoni mwake. [16]
Wanapo pokea wapokeaji wawili, wanao kaa kuliani na kushotoni. [17]
Hatamki neno ila karibu yake yupo mwangalizi tayari. [18]
Na uchungu wa kutoka roho utamjia kwa haki. Hayo ndiyo uliyo kuwa ukiyakimbia. [19]
Na litapulizwa baragumu. Hiyo ndiyo Siku ya Miadi. [20]
Na kila nafsi itakuja na pamoja nayo mchungaji na shahidi. [21]
(Aambiwe): Kwa hakika ulikuwa umeghafilika na haya; basi leo tumekuondolea pazia lako, na kwa hivyo kuona kwako leo ni kukali. [22]
Na mwenzake atasema: Huyu niliye naye mimi kesha tayarishwa. [23]
Mtupeni katika Jahannamu kila kafiri mwenye inda, [24]
Akatazaye kheri, arukaye mipaka, mwenye kutia shaka, [25]
Aliye weka mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu. Basi mtupeni katika adhabu kali. [26]
Mwenzake aseme: Ee Mola wetu Mlezi! Sikumpoteza mimi, bali yeye mwenyewe alikuwa katika upotovu wa mbali. [27]
(Mwenyezi Mungu) aseme: Msigombane mbele yangu. Nilikuleteeni mbele onyo langu. [28]
Mbele yangu haibadilishwi kauli, wala Mimi siwadhulumu waja wangu. [29]
Siku tutapo iambia Jahannamu: Je! Umejaa? Nayo itasema: Je! Kuna ziada? [30]
Na Pepo italetwa karibu kwa ajili ya wachamngu, haitakuwa mbali. [31]
Haya ndiyo mnayo ahidiwa kwa kila mwenye kurejea kwa Mwenyezi Mungu na akajilinda. [32]
Mwenye kumwogopa Mwingi wa Rehema hali kuwa hamwoni, na akaja kwa moyo ulio elekea [33]
(Ataambiwa) ingieni kwa salama. Hiyo ndiyo siku ya daima dawamu. [34]
Humo watapata wakitakacho, na kwetu yako ya ziada. [35]
Na kaumu ngapi tuliziangamiza kabla yao walio kuwa na nguvu zaidi kuliko hawa! Nao walitanga tanga katika nchi nyingi. Je! Walipata pa kukimbilia? [36]
Hakika katika hayo upo ukumbusho kwa mwenye moyo au akatega sikio naye yupo anashuhudia. [37]
Na bila ya shaka Sisi tumeziumba mbingu na ardhi na vilio baina yao mnamo siku sita; na wala hayakutugusa machofu. [38]
Basi vumilia kwa hayo wasemayo, na mtakase kwa kumsifu Mola wako Mlezi kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa. [39]
Na katika usiku pia mtakase, na baada ya kusujudu. [40]
Na sikiliza siku atapo nadi mwenye kunadi kutoka pahala karibu. [41]
Siku watakapo sikia ukelele wa haki. Hiyo ndiyo siku ya kufufuka. [42]
Hakika Sisi tunahuisha na tunafisha, na kwetu Sisi ndio marejeo. [43]
Siku itapo wapasukia ardhi mbio mbio! Mkusanyo huo kwetu ni mwepesi. [44]
Sisi tunajua kabisa wayasemayo. Wala wewe si mwenye kuwatawalia kwa ujabari. Basi mkumbushe kwa Qur'ani anaye liogopa onyo. [45]