The Noble Qur'an Encyclopedia
Towards providing reliable exegeses and translations of the meanings of the Noble Qur'an in the world languagesThe winnowing winds [Adh-Dhariyat] - Swahili translation - Ali Muhsen Al-Berwani
Surah The winnowing winds [Adh-Dhariyat] Ayah 60 Location Maccah Number 51
Naapa kwa pepo zinazo tawanya! [1]
Na zinazo beba mizigo! [2]
Na zinazo kwenda kwa wepesi. [3]
Na zinazo gawanya kwa amri! [4]
Hakika mnayo ahidiwa bila ya shaka ni kweli! [5]
Na kwa hakika malipo bila ya shaka yatatokea. [6]
Naapa kwa mbingu zenye njia! [7]
Hakika nyinyi bila ya shaka mmo katika kauli inayo khitalifiana. [8]
Anageuzwa kutokana na haki mwenye kugeuzwa. [9]
Wazushi wameangamizwa. [10]
Ambao wameghafilika katika ujinga. [11]
Wanauliza: Ni lini hiyo siku ya malipo? [12]
Hiyo ni siku watakayo adhibiwa Motoni. [13]
Onjeni adhabu yenu! Haya ndiyo mliyo kuwa mkiyahimiza. [14]
Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na chemchem. [15]
Wanapokea aliyo wapa Mola wao Mlezi. Kwa hakika hao walikuwa kabla ya haya wakifanya mema. [16]
Walikuwa wakilala kidogo tu usiku. [17]
Na kabla ya alfajiri wakiomba maghfira. [18]
Na katika mali yao ipo haki ya mwenye kuomba na asiye omba. [19]
Na katika ardhi zipo Ishara kwa wenye yakini. [20]
Na pia katika nafsi zenu - Je! Hamwoni? [21]
Na katika mbingu ziko riziki zenu na mliyo ahidiwa. [22]
Basi naapa kwa Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, hakika haya ni kweli kama ilivyo kweli kuwa nyinyi mnasema. [23]
Je! Imekufikia hadithi ya wageni wa Ibrahim wanao hishimiwa? [24]
Walipo ingia kwake wakasema: Salama! Na yeye akasema: Salama! Nyinyi ni watu nisio kujueni. [25]
Akenda kwa ahali yake na akaja na ndama aliye nona. [26]
Akawakaribisha, akasema: Mbona hamli? [27]
Akahisi kuwaogopa katika nafsi yake. Wakasema: Usiwe na khofu, nao wakambashiria kupata kijana mwenye ilimu. [28]
Ndipo mkewe akawaelekea, na huku anasema na akijipiga usoni kwa mastaajabu, na kusema: Mimi ni kikongwe na tasa! [29]
Wakasema: Ndivyo vivyo hivyo alivyo sema Mola wako Mlezi. Hakika Yeye ni Mwenye hikima na Mwenye kujua. [30]
AKASEMA: Basi ujumbe wenu ni nini, enyi mlio tumwa? [31]
Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa watu wakosefu, [32]
Tuwatupie mawe ya udongo, [33]
Yaliyo tiwa alama kutoka kwa Mola wako Mlezi kwa ajili ya wanao pindukia mipaka. [34]
Kwa hivyo tutawatoa katika hao wale walio amini. [35]
Lakini hatukupata humo ila nyumba moja tu yenye Waislamu! [36]
Na tukaacha humo Ishara kwa ajili ya wanao iogopa adhabu chungu. [37]
Na katika khabari za Musa, tulipo mtuma kwa Firauni na hoja wazi. [38]
Lakini alipuuza kwa sababu ya nguvu zake na akasema: Huyu ni mchawi au mwendawazimu! [39]
Basi tukamkamata yeye na majeshi yake na tukawatupa baharini, na yeye ndiye wa kulaumiwa. [40]
Na katika khabari za A'di tulipo wapelekea upepo wa kukata uzazi. [41]
Haukuacha chochote ulicho kifikia ila ulikifanya kama kilio nyambuka. [42]
Na katika khabari za Thamudi walipo ambiwa: Jifurahisheni kwa muda mdogo tu. [43]
Wakaasi amri ya Mola wao Mlezi. Basi uliwanyakua moto wa radi nao wanaona. [44]
Basi hawakuweza kusimama wala hawakuwa wenye kujitetea. [45]
Na kaumu ya Nuhu hapo mbele. Hakika hao walikuwa watu wapotovu. [46]
Na mbingu tumezifanya kwa nguvu na uwezo na hakika Sisi bila ya shaka ndio twenye uwezo wa kuzitanua. [47]
Na ardhi tumeitandaza; basi watandazaji wazuri namna gani Sisi! [48]
Na katika kila kitu tumeumba kwa jozi ili mzingatie. [49]
Basi kimbilieni kwa Mwenyezi Mungu, hakika mimi ni mwonyaji kwenu wa kubainisha nitokae kwake. [50]
Wala msifanye kuwa kuna mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu. Hakika mimi ni mwonyaji kwenu wa kubainisha nitokae kwake. [51]
Basi ndio hivyo hivyo, hakuwajia kabla yao Mtume ila walisema: Huyu ni mchawi au mwendawazimu. [52]
Je! Wameambizana kwa haya? Bali hawa ni watu waasi. [53]
Basi waachilie mbali, nawe hulaumiwi. [54]
Na kumbusha, kwani ukumbusho huwafaa Waumini. [55]
Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi. [56]
Na sitaki kwao riziki, wala sitaki wanilishe.Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuruzuku, Mwenye nguvu, Madhubuti. [57]
Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuruzuku, Mwenye nguvu, Madhubuti. [58]
Hakika walio dhulumu wana fungu lao la adhabu kama fungu la wenzao. Basi wasinihimize. [59]
Ole wao walio ikanusha siku yao waliyo ahidiwa. [60]