The Noble Qur'an Encyclopedia
Towards providing reliable exegeses and translations of the meanings of the Noble Qur'an in the world languagesMount Sinai [At-tur] - Swahili translation - Ali Muhsen Al-Berwani
Surah Mount Sinai [At-tur] Ayah 49 Location Maccah Number 52
Naapa kwa mlima wa T'ur! [1]
Na Kitabu kilicho andikwa . [2]
Katika ngozi iliyo kunjuliwa! [3]
Na kwa Nyumba iliyo jengwa! [4]
Na kwa dari iliyo nyanyuliwa! [5]
Na kwa bahari iliyo jazwa! [6]
Hakika adhabu ya Mola wako Mlezi hapana shaka itatokea. [7]
Hapana wa kuizuia. [8]
Siku zitakapo tikisika mbingu kwa mtikiso! [9]
Na milima iwe inakwenda kwa mwendo mkubwa. [10]
Basi ole wao siku hiyo hao wanao kadhibisha, [11]
Ambao wanacheza katika mambo ya upuuzi. [12]
Siku watapo sukumwa kwenye Moto kwa msukumo wa nguvu, [13]
(Waambiwe): Huu ndio ule Moto mlio kuwa mkiukanusha! [14]
Je! Huu ni uchawi, au hamwoni tu? [15]
Uingieni, mkistahamili au msistahamili - ni mamoja kwenu. Hakika mnalipwa kwa mliyo kuwa mkiyatenda. [16]
Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na neema, [17]
Wakifurahi kwa yale aliyo wapa Mola wao Mlezi. Na Mola wao Mlezi atawalinda na adhabu ya Motoni. [18]
Kuleni na kunyweni kwa raha kabisa kwa sababu ya mliyo kuwa mkiyatenda. [19]
Watakuwa wameegemea juu ya viti vya enzi vilivyo pangwa kwa safu. Na tutawaoza mahuru-l-aini. [20]
Na walio amini na dhuriya zao wakawafuata kwa Imani tutawakutanisha nao dhuriya zao, na wala hatutawapunja hata kidogo katika vitendo vyao. Kila mtu lazima atapata alicho kichuma. [21]
Na tutawapa matunda, na nyama kama watavyo penda. [22]
Watapeana humo bilauri zisio na vinywaji vya kuleta maneno ya upuuzi wala dhambi. [23]
Iwe wanawapitia watumishi wao kama kwamba ni lulu zilizomo katika chaza. [24]
Wataelekeana wakiulizana. [25]
Waseme: Tulikuwa zamani pamoja na ahali zetu tukiogopa; [26]
Basi Mwenyezi Mungu akatufanyia hisani na akatulinda na adhabu ya upepo wa Moto. [27]
Hakika sisi zamani tulikuwa tukimwomba Yeye tu. Hakika Yeye ndiye Mwema Mwenye kurehemu. [28]
Basi kumbusha! Kwani wewe, kwa neema ya Mola wako Mlezi, si kuhani wala mwendawazimu. [29]
Au wanasema: Huyu ni mtunga mashairi, tunamtarajia kupatilizwa na dahari. [30]
Sema: Tarajieni, na mimi pia ni pamoja nanyi katika kutarajia. [31]
Au hizo akili zao ndio zinawaamrisha haya, au wao basi ni watu majeuri tu? [32]
Au ndio wanasema: Ameitunga hii! Bali basi tu hawaamini! [33]
Basi nawalete masimulizi kama haya ikiwa wao wanasema kweli. [34]
Au wao wameumbwa pasipo kutokana na kitu chochote, au ni wao ndio waumbaji? [35]
Au wao wameziumba mbingu na ardhi? Bali hawana na yakini. [36]
Au wanazo khazina za Mola wako Mlezi au wao ndio wenye madaraka? [37]
Au wanazo ngazi za kusikilizia? Basi huyo msikilizaji wao na alete hoja ilio wazi! [38]
Au Yeye Mwenyezi Mungu ana wasichana, na nyinyi ndio mna wavulana? [39]
Au wewe unawaomba ujira, na kwa hivyo ndio wanaelemewa na uzito wa gharama? [40]
Au wanayo ilimu ya ghaibu, nao wameandika? [41]
Au wanataka kufanya vitimbi tu? Lakini hao walio kufuru ndio watakao tegeka. [42]
Au wanae mungu asiye kuwa Mwenyezi Mungu? Subhanallah! Ametaksika Mwenyezi Mungu na hao wanao washirikisha naye. [43]
Na hata wange ona pande linatoka mbinguni linaanguka wange sema: Ni mawingu yaliyo bebana. [44]
Basi waache mpaka wakutane na siku yao watakapo hilikishwa. [45]
Siku ambayo hila zao hazitawafaa hata kidogo, wala wao hawatanusuriwa. [46]
Na hakika walio dhulumu watapata adhabu nyengine isiyo kuwa hii, lakini wengi wao hawajui. [47]
Na ingojee hukumu ya Mola wako Mlezi. Kwani wewe hakika uko mbele ya macho yetu, na mtakase kwa kumsifu Mola wako Mlezi unapo simama, [48]
Na usiku pia mtakase, na zinapo kuchwa nyota. [49]