The Noble Qur'an Encyclopedia
Towards providing reliable exegeses and translations of the meanings of the Noble Qur'an in the world languagesThe moon [Al-Qamar] - Swahili translation - Ali Muhsen Al-Berwani
Surah The moon [Al-Qamar] Ayah 55 Location Maccah Number 54
Saa imekaribia, na mwezi umepasuka! [1]
Na wakiona Ishara hugeuka upande na husema: Huu uchawi tu unazidi kuendelea. [2]
Na wamekanusha na wamefuata matamanio yao. Na kila jambo ni lenye kuthibiti. [3]
Na bila ya shaka zimewajia khabari zenye makaripio. [4]
Hikima kaamili; lakini maonyo hayafai kitu! [5]
Basi jiepushe nao. Siku atakapo ita mwitaji kuliendea jambo linalo chusha; . [6]
Macho yao yatainama; watatoka makaburini kama nzige walio tawanyika! [7]
Wanamkimbilia mwitaji, na makafiri wanasema: Hii ni siku ngumu. [8]
Kabla yao kaumu ya Nuhu walikanusha; wakamkanusha mja wetu, na wakasema ni mwendawazimu, na akakaripiwa. [9]
Basi akamwomba Mola wake Mlezi akasema: Kwa hakika mimi nimeshindwa, basi ninusuru! [10]
Basi tukaifungua milango ya mbingu kwa maji yanayo miminika. [11]
Na tukazipasua ardhi kwa chemchem, yakakutana maji kwa jambo lilio kadiriwa. [12]
Na tukamchukua kwenye safina ya mbao na kamba. [13]
Ikawa inakwenda kwa nadhari yetu, kuwa ni malipo kwa alivyo kuwa amekanushwa. [14]
Na bila ya shaka tuliiacha iwe ni Ishara. Lakini je, yupo anaye kumbuka? [15]
Basi ilikuwaje adhabu yangu, na maonyo yangu. [16]
Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur'ani iwe nyepesi kufahamika. Lakini yupo anaye kumbuka? [17]
Kina A'di walikanusha. Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu? [18]
Hakika Sisi tuliwapelekea upepo wa kimbunga katika siku korofi mfululizo, [19]
Ukiwang'oa watu kama vigogo vya mitende vilio ng'olewa. [20]
Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu? [21]
Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur'ani nyepesi kufahamika; lakini yupo anaye kumbuka? [22]
Thamudi waliwakanusha Waonyaji. [23]
Wakasema: Ati tumfuate binaadamu mmoja katika sisi? Basi hivyo sisi tutakuwa katika upotofu na kichaa! [24]
Ni yeye tu aliye teremshiwa huo ukumbusho kati yetu sote? Bali huyu ni mwongo mwenye kiburi! [25]
Kesho watajua ni nani huyo mwongo mwenye kiburi. [26]
Hakika Sisi tutawapelekea ngamia jike ili kuwajaribu, basi watazame tu na ustahamili. [27]
Na waambie kwamba maji yatagawanywa baina yao; kila sehemu ya maji itahudhuriwa na aliye khusika. [28]
Basi wakamwita mtu wao akaja akamchinja. [29]
Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu! [30]
Hakika Sisi tuliwapelekea ukelele mmoja tu, wakawa kama mabuwa ya kujengea uwa. [31]
Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur'ani iwe nyepesi kwa kukumbuka, lakini yupo akumbukaye? [32]
Kaumu Lut'i nao waliwakadhibisha Waonyaji. [33]
Hakika Sisi tukawapelekea kimbunga cha vijiwe, isipo kuwa wafuasi wa Lut'i. Hao tuliwaokoa karibu na alfajiri. [34]
Kwa neema inayo toka kwetu. Hivyo ndivyo tumlipavyo anaye shukuru. [35]
Na hakika yeye aliwaonya adhabu yetu; lakini wao waliyatilia shaka hayo maonyo. [36]
Na walimtaka awape wageni wake. Tukayapofua macho yao, na tukawaambia: Onjeni basi adhabu na maonyo yangu! [37]
Na iliwafikia wakati wa asubuhi adhabu yangu ya kuendelea. [38]
Basi onjeni adhabu na maonyo yangu!< [39]
Na hakika tumeisahilisha Qur'ani kuikumbuka. Lakini yupo anaye kumbuka? [40]
Na Waonyaji waliwafikia watu wa Firauni. [41]
Walizikadhibisha Ishara zetu zote, nasi tukawashika kama anavyo shika Mwenye nguvu Mwenye uweza. [42]
Je! Makafiri wenu ni bora kuliko hao, au yameandikwa vitabuni kuwa nyinyi hamtiwi makosani? [43]
Au ndio wanasema: Sisi ni wengi tutashinda tu. [44]
Wingi wao huu utashindwa, na wao watasukumwa nyuma. [45]
Bali Saa ya Kiyama ndio miadi yao, na Saa hiyo ni nzito zaidi na chungu zaidi. [46]
Hakika wakosefu wamo katika upotofu na wazimu. [47]
Siku watakapo kokotwa Motoni kifudifudi waambiwe: Onjeni mguso wa Jahannamu! [48]
Kwa hakika Sisi tumekiumba kila kitu kwa kipimo. [49]
Na amri yetu haikuwa ila ni moja tu, kama kupepesa jicho. [50]
Na bila ya shaka tumekwisha waangamiza wenzenu. Lakini yupo anaye kumbuka? [51]
Na kila jambo walilo lifanya limo vitabuni. [52]
Na kila kidogo na kikubwa kimeandikwa. [53]
Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na mito. [54]
Katika makalio ya haki kwa Mfalme Mwenye uweza. [55]