The Noble Qur'an Encyclopedia
Towards providing reliable exegeses and translations of the meanings of the Noble Qur'an in the world languagesThe Event, The Inevitable [Al-Waqia] - Swahili translation - Ali Muhsen Al-Berwani
Surah The Event, The Inevitable [Al-Waqia] Ayah 96 Location Maccah Number 56
Litakapo tukia hilo Tukio . [1]
Hapana cha kukanusha kutukia kwake. [2]
Literemshalo linyanyualo! [3]
Itakapo tikiswa ardhi kwa mtikiso! [4]
Na milima itapo sagwasagwa! [5]
Iwe mavumbi yanayo peperushwa! [6]
Na nyinyi mtakuwa namna tatu: . [7]
Basi watakuwepo wa kuliani; je, ni wepi wa kuliani? [8]
Na wa kushotoni; je, ni wepi wa kushotoni? [9]
Na wa mbele watakuwa mbele. [10]
Hao ndio watakao karibishwa [11]
Katika Bustani zenye neema. [12]
Fungu kubwa katika wa mwanzo, [13]
Na wachache katika wa mwisho. [14]
Watakuwa juu ya viti vya fakhari vilivyo tonewa. [15]
Wakiviegemea wakielekeana. [16]
Wakitumikiwa na wavulana wa ujana wa milele, [17]
Kwa vikombe na mabirika na bilauri za vinywaji kutoka chemchem safi. [18]
Hawataumwa kichwa kwa vinywaji hivyo wala hawatoleweshwa. [19]
Na matunda wayapendayo, [20]
Na nyama za ndege kama wanavyo tamani. [21]
Na Mahurulaini, [22]
Walio kama mfano wa lulu zilio hifadhiwa. [23]
Ni malipo kwa waliyo kuwa wakiyatenda. [24]
Humo hawatasikia porojo wala maneno ya dhambi, [25]
Isipo kuwa maneno ya Salama, Salama. [26]
Na wale wa mkono wa kulia, ni yepi yatakuwa ya wa kuliani? [27]
Katika mikunazi isiyo na miba, [28]
Na migomba iliyo pangiliwa, [29]
Na kivuli kilicho tanda, [30]
Na maji yanayo miminika, [31]
Na matunda mengi, [32]
Hayatindikii wala hayakatazwi, [33]
Na matandiko yaliyo nyanyuliwa. [34]
Hakika Sisi tutawaumba (Mahurulaini) upya, [35]
Na tutawafanya vijana, [36]
Wanapendana na waume zao, hirimu moja. [37]
Kwa ajili ya watu wa kuliani. [38]
Fungu kubwa katika wa mwanzo, [39]
Na fungu kubwa katika wa mwisho. [40]
Na watu wa kushotoni; je ni yepi ya wa kushotoni? [41]
Katika upepo wa moto, na maji yanayo chemka, [42]
Na kivuli cha moshi mweusi, [43]
Si cha kuburudisha wala kustarehesha. [44]
Hakika hao walikuwa kabla ya haya wakiishi maisha ya anasa. [45]
Na walikuwa wakishikilia kufanya madhambi makubwa, [46]
Na walikuwa wakisema: Tutakapo kufa na tukawa udongo na mafupa, ati ndio tutafufuliwa? [47]
Au baba zetu wa zamani? [48]
Sema: Hakika wa zamani na wa mwisho [49]
Bila ya shaka watakusanywa kwa wakati wa siku maalumu. [50]
Kisha nyinyi, mlio potea, mnao kanusha, [51]
Kwa yakini mtakula mti wa Zaqqumu. [52]
Na kwa mti huo mtajaza matumbo. [53]
Na juu yake mtakunywa maji yanayo chemka. [54]
Tena mtakunywa kama wanavyo kunywa ngamia wenye kiu. [55]
Hiyo ndiyo karamu yao Siku ya Malipo. [56]
Sisi tumekuumbeni; basi hamsadiki? [57]
Je! Mnaiona mbegu ya uzazi mnayo idondokeza? [58]
Je! Mnaiumba nyinyi, au ni Sisi ndio Waumbaji? [59]
Sisi tumekuwekeeni mauti; na wala Sisi hatushindwi [60]
Kuwaleta wengine badala yenu na kukuumbeni nyinyi kwa umbo msilo lijua. [61]
Na bila ya shaka mlikwisha jua umbo la kwanza, basi kwa nini hamkumbuki? [62]
Je! Mnaona makulima mnayo yapanda? [63]
Je! Ni nyinyi mnayo yaotesha au ni Sisi ndio wenye kuotesha? [64]
Tungeli taka tungeli yafanya yakawa mapepe, mkabaki mnastaajabu, [65]
Mkisema: Hakika sisi tumegharimika; [66]
Bali sisi tumenyimwa. [67]
Je! Mnayaona maji mnayo yanywa? [68]
Je! Ni nyinyi mnayo yateremsha kutoka mawinguni au ni Sisi ndio wenye kuyateremsha? [69]
Tungeli penda tungeli yafanya ya chumvi. Basi mbona hamshukuru? [70]
Je! Mnauona moto mnao uwasha? [71]
Ni nyinyi mlio uumba mti wake au Sisi ndio Waumbaji? [72]
Sisi tumeufanya uwe ni ukumbusho na manufaa kwa walioko nyikani. [73]
Basi litakase jina la Mola wako Mlezi aliye Mkuu. [74]
Basi naapa kwa maanguko ya nyota, [75]
Na hakika bila ya shaka hichi ni kiapo kikubwa, laiti mngeli jua! [76]
Hakika hii bila ya shaka ni Qur'ani Tukufu, [77]
Katika Kitabu kilicho hifadhiwa. [78]
Hapana akigusaye ila walio takaswa. [79]
Ni uteremsho unao toka kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. [80]
Ni maneno haya ndiyo nyinyi mnayapuuza? [81]
Na badala ya kushukuru kwa riziki yenu mnafanya kuwa mnakadhibisha? [82]
Yawaje basi itakapo fika roho kwenye koo, [83]
Na nyinyi wakati huo mnatazama! [84]
Na Sisi tuko karibu zaidi naye kuliko nyinyi. [85]
Na lau kuwa nyinyi hamumo katika mamlaka yangu, [86]
Kwanini hamuirudishi hiyo roho, ikiwa nyinyi mnasema kweli? [87]
Basi akiwa miongoni mwa walio karibishwa, [88]
Basi ni raha, na manukato, na Bustani zenye neema. [89]
Na akiwa katika watu wa upande wa kulia, [90]
Basi ni Salamu kwako uliye miongoni mwa watu wa upande wa kulia. [91]
Na ama akiwa katika walio kadhibisha wapotovu, [92]
Basi karamu yake ni maji yanayo chemka, [93]
Na kutiwa Motoni. [94]
Hakika hii ndiyo haki yenye yakini. [95]
Basi litakase jina la Mola wako Mlezi aliye Mkubwa. [96]