The Noble Qur'an Encyclopedia
Towards providing reliable exegeses and translations of the meanings of the Noble Qur'an in the world languagesThe Hypocrites [Al-Munafiqoon] - Swahili translation - Ali Muhsen Al-Berwani
Surah The Hypocrites [Al-Munafiqoon] Ayah 11 Location Madanah Number 63
Wanapo kujia wanaafiki husema: Tunashuhudia ya kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anajua kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu anashuhudia ya kuwa hakika wanaafiki ni waongo. [1]
Wamevifanya viapo vyao ni kinga, na wao wakajizuia kuifuata Njia ya Mwenyezi Mungu. Hakika ni mabaya kabisa waliyo kuwa wakiyafanya. [2]
Hayo ni kwa sababu ya kuwa waliamini, kisha wakakufuru; kwa hivyo umepigwa muhuri juu ya nyoyo zao. Kwa hivyo hawafahamu lolote. [3]
Na unapo waona, miili yao inakupendeza, na wakisema, unasikiliza usemi wao. Lakini wao ni kama magogo yaliyo egemezwa. Wao hudhania kila ukelele unao pigwa ni kwa ajili yao. Hao ni maadui; tahadhari nao. Mwenyezi Mungu awaangamizilie mbali! Vipi wanapotoka na haki? [4]
Na wanapo ambiwa: Njooni ili Mtume wa Mwenyezi Mungu akuombeeni maghfira, huvigeuza vichwa vyao, na unawaona wanageuka nao wamejaa kiburi. [5]
Sawa sawa kwao, ukiwatakia maghfira au hukuwatakia maghfira, Mwenyezi Mungu hatawaghufiria. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wapotovu. [6]
Hao ndio wanao sema: Msitoe mali kwa ajili ya walioko kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, ili waondokelee mbali! Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye khazina za mbingu na ardhi, lakini wanaafiki hawafahamu. [7]
Wanasema: Tukirejea Madina mwenye utukufu zaidi bila ya shaka atamfukuza aliye mnyonge. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye utukufu - Yeye, na Mtume wake, na Waumini. Lakini wanaafiki hawajui. [8]
Enyi mlio amini! Yasikusahaulisheni mali yenu, wala watoto wenu, kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Na wenye kufanya hayo ndio walio khasiri. [9]
Na toeni katika tulicho kupeni kabla hayajamfikia mmoja wenu mauti, tena hapo akasema: Mola wangu Mlezi! Huniakhirishi muda kidogo nipate kutoa sadaka, na niwe katika watu wema? [10]
Wala Mwenyezi Mungu hataiakhirisha nafsi yoyote inapo fika ajali yake; na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda. [11]