The Noble Qur'an Encyclopedia
Towards providing reliable exegeses and translations of the meanings of the Noble Qur'an in the world languagesThe Sovereignty [Al-Mulk] - Swahili translation - Ali Muhsen Al-Berwani
Surah The Sovereignty [Al-Mulk] Ayah 30 Location Maccah Number 67
AMETUKUKA ambaye mkononi mwake umo Ufalme wote; na Yeye ni Mwenye uweza juu ya kila kitu. [1]
Ambaye ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi. Na Yeye ni Mwenye nguvu na Mwenye msamaha. [2]
Aliye umba mbingu saba kwa matabaka. Huoni tafauti yoyote katika uumbaji wa Mwingi wa Rehema. Hebu rudisha nadhari! Unaona kosa lolote? [3]
Tena rudisha nadhari mara mbili, nadhari yako itakurejea mwenyewe hali ya kuwa imehizika nayo imechoka. [4]
Na kwa hakika tumeipamba mbingu ya karibu kwa mataa, na tumeyafanya ili kuwapigia mashetani, na tumewaandalia adhabu ya Moto uwakao kwa nguvu. [5]
Na kwa walio mkufuru Mola wao Mlezi ipo adhabu ya Jahannamu. Na ni marejeo maovu yalioje hayo! [6]
Watakapo tupwa humo watausikia mngurumo wake na huku inafoka. [7]
Inakaribia kupasuka kwa hasira. Kila mara likitupwa kundi humo walinzi wake huwauliza: Kwani hakukujieni mwonyaji? [8]
Watasema: Kwani! Ametujia mwonyaji, lakini tulimkadhibisha, na tukasema: Mwenyezi Mungu hakuteremsha chochote. Nyinyi hamumo ila katika upotovu mkubwa! [9]
Na watasema: Lau kuwa tungeli sikia, au tungeli kuwa na akili, tusingeli kuwa katika watu wa Motoni! [10]
Wakakiri dhambi zao. Basi kuangamia ni kwa watu wa Motoni! [11]
Hakika wanao mwogopa Mola wao Mlezi kwa ghaibu, watapata maghfira na ujira mkubwa. [12]
Na ficheni kauli zenu, au zitangazeni; hakika Yeye ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani. [13]
Asijue aliye umba, naye ndiye Mjua siri, Mwenye khabari? [14]
Yeye ndiye aliye idhalilisha ardhi kwa faida yenu, basi tembeeni katika pande zake, na kuleni katika riziki zake. Na kwake Yeye ndio kufufuliwa. [15]
Mnadhani mko salama kwa alioko juu kuwa hatakudidimizeni kwenye ardhi, na tahamaki hiyo inatikisika! [16]
Au mnadhani mko salama kwa alioko juu ya kuwa Yeye hakupelekeeni kimbunga chenye changarawe? Mtajua vipi maonyo yangu? [17]
Na bila ya shaka walikwisha kanusha walio kuwa kabla yao; basi kulikuwaje kukasirika kwangu? [18]
Kwani hawawaoni ndege walioko juu yao namna wanavyo zikunjua mbawa zao, na kuzikunja? Hawawashikilii ila Mwingi wa rehema. Hakika Yeye ni Mwenye kuona kila kitu. [19]
Au ni lipi hilo jeshi lenu la kukunusuruni badala ya Mwingi wa Rehema? Hakika makafiri hawamo ila katika udanganyifu. [20]
Au ni nani huyo ambaye atakupeni riziki kama Yeye akizuia riziki yake? Bali wao wanakakamia tu katika jeuri na chuki. [21]
Je! Anaye kwenda akisinukia juu ya uso wake ni mwongofu zaidi, au yule anaye kwenda sawasawa katika Njia Iliyo Nyooka? [22]
Sema: Yeye ndiye aliye kuumbeni tangu mwanzo, na akakupeni masikio na macho, na nyoyo. Ni kidogo kabisa shukrani zenu. [23]
Sema: Yeye ndiye aliye kutawanyeni katika ardhi, na kwake mtakusanywa. [24]
Na wanasema: Lini ahadi hii, ikiwa mnasema kweli? [25]
Sema: Hakika ujuzi wake uko kwa Mwenyezi Mungu; na hakika mimi ni mwonyaji tu mwenye kubainisha. [26]
Lakini watakapo iona karibu, nyuso za walio kufuru zitahuzunishwa, na itasemwa: Hayo ndiyo mliyo kuwa mkiyaomba. [27]
Sema: Mwaonaje, ikiwa Mwenyezi Mungu atanihiliki mimi na walio pamoja nami, au akiturehemu, ni nani atakaye walinda makafiri na adhabu chungu? [28]
Sema: Yeye ndiye Mwingi wa Rehema; tunamuamini Yeye, na juu yake tunategemea. Mtakuja jua ni nani aliye katika upotovu ulio dhaahiri. [29]
Sema: Mwaonaje, yakiwa maji yenu yamedidimia chini, nani atakueleteeni maji yanayo miminika? [30]