The Noble Qur'an Encyclopedia
Towards providing reliable exegeses and translations of the meanings of the Noble Qur'an in the world languagesThe Pen [Al-Qalam] - Swahili translation - Ali Muhsen Al-Berwani
Surah The Pen [Al-Qalam] Ayah 52 Location Maccah Number 68
Nuun. Naapa kwa kalamu na yale wayaandikayo! [1]
Kwa neema ya Mola wako Mlezi wewe si mwendawazimu. [2]
Na kwa hakika wewe una malipo yasiyo katika. [3]
Na hakika wewe una tabia tukufu. [4]
Karibu utaona, na wao wataona! [5]
Ni nani kati yenu aliye pandwa na wazimu. [6]
Hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye ajuaye zaidi nani aliye ipotea Njia yake, na Yeye ndiye anaye wajua zaidi walio ongoka. [7]
Basi usiwat'ii wanao kadhibisha. [8]
Wanatamani lau unge lainisha ili nao wakulainishie. [9]
Wala usimt'ii kila mwingi wa kuapa wa kudharauliwa, [10]
Mtapitapi apitae akifitini. [11]
Mwenye kuzuia kheri, dhaalimu, mwingi wa madhambi, [12]
Mkavu, na juu ya hayo, mshari, amejipachika tu. [13]
Ati kwa kuwa ana mali na watoto! [14]
Anapo somewa Aya zetu, husema: Hizi ni simulizi za uwongo za watu wa zamani! [15]
Tutamtia kovu juu ya pua yake. [16]
Hakika tumewajaribu hawa kama tulivyo wajaribu wale wenye shamba, walipo apa kwamba watayavuna mazao yake itakapo kuwa asubuhi. [17]
Wala hawakusema: Mungu akipenda! [18]
Basi lilitokea tukio juu yake kutoka kwa Mola wako Mlezi, nao wamelala! [19]
Likawa kama usiku wa giza. [20]
Asubuhi wakaitana. [21]
Ya kwamba nendeni kondeni mwenu ikiwa mnataka kuvuna. [22]
Basi walikwenda na huku wakinong'onezana, [23]
Ya kuwa leo hata masikini mmoja asikuingilieni. [24]
Na walikwenda asubuhi, nao wameshikilia azimio hilo. [25]
Basi walipo liona, wakasema: Hakika tumepotea! [26]
Bali tumenyimwa! [27]
Mbora wao akasema: Sikukwambieni, kwa nini hamumtakasi Mwenyezi Mungu? [28]
Wakasema: Ametakasika Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tulikuwa wenye kudhulumu. [29]
Basi wakakabiliana kulaumiana wao kwa wao. [30]
Wakasema: Ole wetu! Tulikuwa tumeikiuka mipaka! [31]
Asaa Mola wetu Mlezi akatubadilishia lilio bora kuliko hili. Hakika sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu Mlezi. [32]
Namna hivi yanakuwa mateso, na bila ya shaka mateso ya Akhera ni makubwa zaidi, laiti wangeli jua! [33]
Hakika wachamngu watakuwa na Bustani za neema kwa Mola wao Mlezi. [34]
Kwani tutawafanya Waislamu kama wakosefu? [35]
Mna nini? Mnahukumu vipi? [36]
Au mnacho kitabu ambacho ndani yake mnasoma? [37]
Kuwa mtapata humo mnayo yapenda? [38]
Au mnazo ahadi za viapo juu yetu za kufika Siku ya Kiyama ya kuwa hakika mtapata kila mnayo jihukumia? [39]
Waulize: Ni nani miongoni mwao dhamini wa haya? [40]
Au wanao washirika? Basi wawalete washirika wao wakiwa wanasema kweli. [41]
Siku utakapo wekwa wazi mundi, na wataitwa kusujudu, lakini hawataweza, [42]
Macho yao yatainama chini, fedheha itawafunika. Na hakika walikuwa wakiitwa wasujudu walipo kuwa wazima [43]
Basi niache na wanao kadhibisha maneno haya! Tutawavutia kidogo kidogo kwa mahali wasipo pajua. [44]
Na ninawapururia muhula; hakika hila zangu ni imara. [45]
Au unawaomba ujira, na wao wanaemewa na gharama hiyo? [46]
Au iko kwao siri, basi wao wanaiandika? [47]
Basi ingojee hukumu ya Mola wako Mlezi, wala usiwe kama mmezwa na samaki, alipo nadi naye kazongwa. [48]
Kama isingeli mfikia neema kutoka kwa Mola wake Mlezi, bila ya shaka angeli tupwa ufukweni naye ni mwenye kulaumiwa. [49]
Lakini Mola wake Mlezi alimteua na akamfanya miongoni mwa watu wema. [50]
Na walio kufuru hukaribia kukutelezesha kwa macho yao, wanapo sikia mawaidha, na wanasema: Hakika yeye ni mwendawazimu. [51]
Na hayakuwa haya, ila ni ukumbusho kwa walimwengu wote. [52]