The Noble Qur'an Encyclopedia
Towards providing reliable exegeses and translations of the meanings of the Noble Qur'an in the world languagesThe reality [Al-Haaqqa] - Swahili translation - Ali Muhsen Al-Berwani
Surah The reality [Al-Haaqqa] Ayah 52 Location Maccah Number 69
Tukio la haki. [1]
Nini hilo Tukio la haki? [2]
Na nini kitakujuulisha nini hilo Tukio la haki? [3]
Thamudi na A'di waliukadhibisha Msiba unao situsha. [4]
Basi Thamudi waliangamizwa kwa balaa kubwa mno. [5]
Na ama A'di waliangamizwa kwa upepo mkali usio zuilika. [6]
Alio wapelekea masiku saba, na siku nane, mfululizo bila ya kusita. Utaona watu wamepinduka kama kwamba ni magongo ya mitende yalio wazi ndani. [7]
Basi je! Unamwona mmoja wao aliye baki? [8]
Na Firauni na walio mtangulia, na miji iliyo pinduliwa chini juu, walileta khatia. [9]
Wakamuasi Mtume wa Mola wao Mlezi, ndipo Yeye Mola akawakamata kwa mkamato ulio zidi nguvu. [10]
Maji yalipo furika Sisi tulikupandisheni katika safina, [11]
Ili tuyafanye hayo kuwa ni waadhi kwenu na kila sikio linalo sikia liyahifadhi. [12]
. Na litapo pulizwa barugumu mpulizo mmoja tu, [13]
Na ardhi na milima ikaondolewa, na ikavunjwa kwa mvunjo mmoja, [14]
Siku hiyo ndio Tukio litatukia. [15]
Na mbingu zitapasuka, kwani siku hiyo zitakuwa dhaifu kabisa. [16]
Na Malaika watakuwa pembezoni mwa mbingu; na wanane juu ya hawa watakuwa wamebeba Kiti cha Enzi cha Mola wako Mlezi. [17]
Siku hiyo mtahudhurishwa - haitafichika siri yoyote yenu. [18]
Basi ama atakaye pewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, atasema: Haya someni kitabu changu! [19]
Hakika nalijua ya kuwa nitapokea hisabu yangu. [20]
Basi yeye atakuwa katika maisha ya kupendeza, [21]
Katika Bustani ya juu, [22]
Matunda yake yakaribu. [23]
Waambiwe: Kuleni na mnywe kwa furaha kwa sababu ya mlivyo tanguliza katika siku zilizo pita. [24]
Na ama atakaye pewa kitabu chake katika mkono wake wa kushoto, basi yeye atasema: Laiti nisingeli pewa kitabu changu! [25]
Wala nisingeli jua nini hisabu yangu. [26]
Laiti mauti ndiyo yangeli kuwa ya kunimaliza kabisa. [27]
Mali yangu hayakunifaa kitu. [28]
Madaraka yangu yamenipotea. [29]
(Pasemwe): Mshikeni! Mtieni pingu! [30]
Kisha mtupeni Motoni! [31]
Tena mtatizeni katika mnyororo wenye urefu wa dhiraa sabiini! [32]
Kwani huyo hakika alikuwa hamuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu, [33]
Wala hahimizi kulisha masikini. [34]
Basi leo hapa hana jamaa wa kumwonea uchungu, [35]
Wala hana chakula ila usaha wa watu wa Motoni. [36]
Chakula hicho hawakili ila wakosefu. [37]
Basi naapa kwa mnavyo viona, [38]
Na msivyo viona, [39]
Kwa hakika hii ni kauli iliyo letwa na Mjumbe mwenye hishima. [40]
Wala si kauli ya mtunga mashairi. Ni machache sana mnayo yaamini. [41]
Wala si kauli ya kuhani. Ni machache mnayo yakumbuka. [42]
Ni uteremsho utokao kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. [43]
Na lau kama angeli tuzulia baadhi ya maneno tu, [44]
Bila ya shaka tungeli mshika kwa mkono wa kulia, [45]
Kisha kwa hakika tungeli mkata mshipa mkubwa wa moyo! [46]
Na hapana yeyote katika nyinyi ambaye angeli weza kutuzuia. [47]
Kwa hakika hii ni mawaidha kwa wachamngu. [48]
Na hakika Sisi bila ya shaka tunajua kwamba miongoni mwenu wapo wanao kadhibisha. [49]
Na hakika bila ya shaka itakuwa ni majuto kwa wanao kataa. [50]
Na hakika hii bila ya shaka ni haki ya yakini. [51]
Basi litakase jina la Mola wako Mlezi Mtukufu. [52]