The Noble Qur'an Encyclopedia
Towards providing reliable exegeses and translations of the meanings of the Noble Qur'an in the world languagesThe Ascending stairways [Al-Maarij] - Swahili translation - Ali Muhsen Al-Berwani
Surah The Ascending stairways [Al-Maarij] Ayah 44 Location Maccah Number 70
Muulizaji aliuliza juu ya adhabu itakayo tokea! [1]
Kwa makafiri - ambayo hapana awezaye kuizuia . [2]
Kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenye mbingu za daraja. [3]
Malaika na Roho hupanda kwendea kwake katika siku ambayo kadiri yake ni miaka khamsini elfu! [4]
Basi subiri kwa subira njema.Hakika wao wanaiona iko mbali! [5]
Hakika wao wanaiona iko mbali! [6]
Na Sisi tunaiona iko karibu. [7]
Siku ambayo mbingu zitakapo kuwa kama maadeni iliyo yayushwa. [8]
Na milima itakuwa kama sufi. [9]
Wala jamaa hatamuuliza jamaa yake. [10]
Ijapo kuwa wataonyeshwa waonane. Atatamani mkosefu lau ajikomboe na adhabu ya siku hiyo kwa kuwatoa fidia wanawe, [11]
Na mkewe, na nduguye, [12]
Na jamaa zake walio kuwa wakimkimu, [13]
Na wote waliomo duniani, kisha aokoke yeye. [14]
La, hasha! Kwa hakika huo ni Moto mkali kabisa, [15]
Unao babua ngozi ya kichwa! [16]
Utamwita kila aliye geuza mgongo na akageuka. [17]
Na akakusanya mali, kisha akayahifadhi. [18]
Hakika mtu ameumbwa na papara. [19]
Inapo mgusa shari hupapatika. [20]
Na inapo mgusa kheri huizuilia. [21]
Isipo kuwa wanao swali, [22]
Ambao wanadumisha Sala zao, [23]
Na ambao katika mali yao iko haki maalumu [24]
Kwa mwenye kuomba na anaye jizuilia kuomba; [25]
Na ambao wanaisadiki Siku ya Malipo, [26]
Na ambao wanaiogopa adhabu itokayo kwa Mola wao Mlezi. [27]
Hakika adhabu ya Mola wao Mlezi si ya kuaminika nayo. [28]
Na ambao wanahifadhi tupu zao. [29]
Isipo kuwa kwa wake zao, au iliyo wamiliki mikono yao ya kuume, basi hao hawalaumiwi [30]
Lakini wanao taka kinyume ya haya, basi hao ndio wanao ruka mipaka. [31]
Na ambao wanazichunga amana zao na ahadi zao, [32]
Na ambao wanasimama imara katika ushahidi wao, [33]
Na ambao wanazihifadhi Sala zao. [34]
Hao ndio watakao hishimiwa Peponi. [35]
Wana nini wale walio kufuru wanakutumbulia macho tu? [36]
Makundi kwa makundi upande wa kulia na upande wa kushoto! [37]
Kwani kila mmoja wao anatumai kuingizwa katika Pepo ya neema? [38]
La, hasha! Hakika Sisi tumewaumba kutokana na wanacho kijua. [39]
Basi naapa kwa Mola Mlezi wa mashariki zote na magharibi zote kwamba Sisi tunaweza [40]
Kuwabadili kwa walio bora kuliko wao; na Sisi hatushindwi. [41]
Basi waache wapige porojo na wacheze, mpaka wakutane na siku yao wanayo ahidiwa, [42]
Siku watakapotoka makaburini kwa upesi kama kwamba wanakimbilia mfundo, [43]
Macho yao yatainama, fedheha itawafunika. Hiyo ndiyo Siku waliyo kuwa wakiahidiwa. [44]