The Noble Qur'an Encyclopedia
Towards providing reliable exegeses and translations of the meanings of the Noble Qur'an in the world languagesThe rising of the dead [Al-Qiyama] - Swahili translation - Ali Muhsen Al-Berwani
Surah The rising of the dead [Al-Qiyama] Ayah 40 Location Maccah Number 75
Ninaapa kwa Siku ya Kiyama! [1]
Na ninaapa kwa nafsi inayo jilaumu! [2]
Anadhani mtu kuwa Sisi hatutaikusanya mifupa yake? [3]
Kwani! Sisi tunaweza hata kuziweka sawa sawa ncha za vidole vyake! [4]
Lakini mtu anataka tu kuendelea na maasi kwa siku zilioko mbele yake. [5]
Anauliza: Lini itakuwa hiyo Siku ya Kiyama? [6]
Basi jicho litapo dawaa! [7]
Na mwezi utapo patwa! [8]
Na likakusanywa jua na mwezi! [9]
Siku hiyo mtu atasema: Yako wapi makimbilio? [10]
La! Hapana pa kukimbilia! [11]
Siku hiyo pa kutua ni kwa Mola wako Mlezi tu. [12]
Siku hiyo ataambiwa aliyo yatanguliza na aliyo yaakhirisha. [13]
Bali mtu ni hoja juu ya nafsi yake. [14]
Na ingawa atatoa chungu ya udhuru. [15]
Usiutikisie huu wahyi ulimi wako kwa kuufanyia haraka. [16]
Hakika ni juu yetu kuukusanya na kuusomesha. [17]
Tunapo usoma, basi nawe fuatiliza kusoma kwake. [18]
Kisha ni juu yetu kuubainisha. [19]
Hasha! Bali nyinyi mnapenda maisha ya duniani, [20]
Na mnaacha maisha ya Akhera. [21]
Zipo nyuso siku hiyo zitao ng'ara, [22]
Zinamwangallia Mola wao Mlezi. [23]
Na zipo nyuso siku hiyo zitakao kunjana. [24]
Zitajua ya kuwa zitafikiwa na livunjalo uti wa mgongo. [25]
La, hasha! (Roho) itakapo fikia kwenye mafupa ya koo, [26]
Na pakasemwa: Nani wa kumganga? [27]
Na mwenyewe akajua kwa hakika kuwa huko ndiko kufariki; [28]
Na utapo ambatishwa muundi kwa muundi, [29]
Siku hiyo ndiyo kuchungwa kupelekwa kwa Mola wako Mlezi! [30]
Kwa sababu hakusadiki, wala hakuswali. [31]
Bali alikanusha, na akageuka. [32]
Kisha akenda kwa ahali zake kwa matao. [33]
Ole wako, ole wako! [34]
Kisha Ole wako, ole wako! [35]
Ati anadhani binaadamu kuwa ataachwa bure? [36]
Kwani hakuwa yeye tone ya manii lilio shushwa? [37]
Kisha akawa kidonge cha damu, tena Mwenyezi Mungu akamuumba na akamtengeneza vilivyo. [38]
Kisha akamfanya namna mbili, mwanamume na mwanamke. [39]
Je! Huyo hakuwa ni Muweza wa kufufua wafu? [40]