The Noble Qur'an Encyclopedia
Towards providing reliable exegeses and translations of the meanings of the Noble Qur'an in the world languagesThe man [Al-Insan] - Swahili translation - Ali Muhsen Al-Berwani
Surah The man [Al-Insan] Ayah 31 Location Madanah Number 76
Hakika kilimpitia binaadamu kipindi katika zama ambacho kwamba hakuwa kitu kinacho tajwa. [1]
Hakika Sisi tumemuumba mtu kutokana na mbegu ya uhai iliyo changanyika, tumfanyie mtihani. Kwa hivyo tukamfanya mwenye kusikia, mwenye kuona. [2]
Hakika Sisi tumembainishia Njia. Ama ni mwenye kushukuru, au mwenye kukufuru. [3]
Hakika HaSisi tumewaandalia makafiri minyororo na pingu na Moto mkali. [4]
Hakika watu wema watakunywa katika vinywaji vilivyo changanyika na kafuri! [5]
Ni chemchem watakao inywa waja wa Mwenyezi Mungu, wakiifanya imiminike kwa wingi. [6]
Wanatimiza ahadi,na wanaiogopa siku ambayo shari yake inaenea sana, [7]
Na huwalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini, na yatima, na wafungwa. [8]
Hakika sisi tunakulisheni kwa wajihi wa Mwenyezi Mungu. Hatutaki kwenu malipo wala shukrani. [9]
Hakika sisi tunaiogopa kwa Mola wetu Mlezi hiyo siku yenye shida na taabu. [10]
Basi Mwenyezi Mungu atwalinda na shari ya siku hiyo, na atawakutanisha na raha na furaha. [11]
Na atawajazi Bustani za Peponi na maguo ya hariri kwa vile walivyo subiri. [12]
Humo wataegemea juu ya viti vya enzi, hawataona humo jua kali wala baridi kali. [13]
Na vivuli vyake vitakuwa karibu yao, na mashada ya matunda yataning'inia mpaka chini. [14]
Na watapitishiwa vyombo vya fedha na vikombe vya vigae, [15]
Vya fedha safi kama kiyoo, wamevipima kwa vipimo. [16]
Na humo watanyweshwa kinywaji kilicho changanyika na tangawizi. [17]
Hiyo ni chemchem iliyo humo inaitwa Salsabil. [18]
Na watawazungukia kuwatumikia wavulana wasio pevuka, ukiwaona utawafikiri ni lulu zilizo tawanywa. [19]
Na utakapo yaona, utakuwa umeona neema na ufalme mkubwa. [20]
Juu yao zipo nguo za hariri laini za kijani kibichi, na hariri nzito ya at'ilasi. Na watavikwa vikuku vya fedha, na Mola wao Mlezi atawanywesha kinywaji safi kabisa. [21]
Hakika haya ni malipo yenu; na juhudi zenu zimekubaliwa. [22]
Hakika Sisi tumekuteremshia Qur'ani kidogo kidogo. [23]
Basi ngojea hukumu ya Mola wako Mlezi wala usimt'ii miongoni mwao mwenye dhambi au mwenye kufuru. [24]
Na likumbuke jina la Mola wako Mlezi asubuhi na jioni; [25]
Na usiku msujudie Yeye, na umtakase usiku, wakati mrefu. [26]
Kwa hakika watu hawa wanapenda maisha ya kidunia, na wanaiacha nyuma yao siku nzito. [27]
Sisi tumewaumba, na tukavitia nguvu viungo vyao. Na tukitaka tutawabadilisha mfano wao wawe badala yao. [28]
Hakika haya ni mawaidha; basi anaye taka atashika Njia ya kwenda kwa Mola wake Mlezi. [29]
Wala hamwezi kutaka ila atakapo Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye ilimu, Mwenye hikima. [30]
Humuingiza amtakaye katika rehema yake. Na wenye kudhulumu amewawekea adhabu iliyo chungu. [31]