The Noble Qur'an Encyclopedia
Towards providing reliable exegeses and translations of the meanings of the Noble Qur'an in the world languagesHe Frowned [Abasa] - Swahili translation - Ali Muhsen Al-Berwani
Surah He Frowned [Abasa] Ayah 42 Location Maccah Number 80
Alikunja kipaji na akageuka! [1]
Kwa sababu alimjia kipofu! [2]
Na nini kitakujuulisha pengine yeye atatakasika? [3]
Au atawaidhika, na mawaidha yamfae? [4]
Ama ajionaye hana haja! [5]
Wewe ndio unamshughulikia? [6]
Na si juu yako kama hakutakasika. [7]
Ama anaye kujia kwa juhudi . [8]
Naye anaogopa! [9]
Ndio wewe unampuuza? [10]
Sivyo hivyo! Huku ni kukumbushana. [11]
Basi anaye penda akumbuke. [12]
Yamo katika kurasa zilizo hishimiwa, [13]
Zilizo inuliwa, zilizo takaswa. [14]
Zimo mikononi mwa Malaika waandishi, [15]
Watukufu, wema. [16]
Ameangamia mwanaadamu! Nini kinacho mkufurisha? [17]
Kwa kitu gani amemuumba? [18]
Kwa tone la manii, akamuumba na akamkadiria. [19]
Kisha akamsahilishia njia. [20]
Kisha akamfisha, akamtia kaburini. [21]
Kisha apendapo atamfufua. [22]
La! Hajamaliza aliyo muamuru. [23]
Hebu mtu na atazame chakula chake. [24]
Hakika Sisi tumemimina maji kwa nguvu, [25]
Tena tukaipasua pasua ardhi kwa nguvu, [26]
Kisha tukaotesha humo nafaka, [27]
Na zabibu, na mimea ya majani, [28]
Na mizaituni, na mitende, [29]
Na bustani zenye miti iliyo songana baraabara, [30]
Na matunda, na malisho ya wanyama; [31]
Kwa manufaa yenu na mifugo yenu. [32]
Basi utakapo kuja ukelele, [33]
Siku ambayo mtu atamkimbia nduguye, [34]
Na mamaye na babaye, [35]
Na mkewe na wanawe. [36]
Kila mtu miongoni mwao siku hiyo atakuwa na lake la kumtosha [37]
Siku hiyo ziko nyuso zitazo nawiri, [38]
Zitacheka, zitachangamka; [39]
Na nyuso siku hiyo zitakuwa na mavumbi, [40]
Giza totoro litazifunika, [41]
Hao ndio makafiri watenda maovu [42]