The Noble Qur'an Encyclopedia
Towards providing reliable exegeses and translations of the meanings of the Noble Qur'an in the world languagesThe Overthrowing [At-Takwir] - Swahili translation - Ali Muhsen Al-Berwani
Surah The Overthrowing [At-Takwir] Ayah 29 Location Maccah Number 81
Jua litakapo kunjwa! [1]
Na nyota zikazimwa! [2]
Na milima ikaondolewa! [3]
Na ngamia wenye mimba pevu watakapo achwa wasishughulikiwe, [4]
Na wanyama wa mwituni wakakusanywa! [5]
Na bahari zikawaka moto! [6]
Na nafsi zikaunganishwa! [7]
Na msichana aliye zikwa hai atapo ulizwa! [8]
Kwa kosa gani aliuliwa? [9]
Na madaftari yatakapo enezwa, [10]
Na mbingu itapo tanduliwa, [11]
Na Jahannamu itapo chochewa, [12]
Na Pepo ikasogezwa, [13]
Kila nafsi itajua ilicho kihudhurisha. [14]
Naapa kwa nyota zinapo rejea nyuma, [15]
Zinazo kwenda, kisha zikajificha, [16]
Na kwa usiku unapo pungua, [17]
Na kwa asubuhi inapo pambazuka, [18]
Kwamba hakika bila ya shaka hii ni kauli ya Mjumbe mtukufu, [19]
Mwenye nguvu na mwenye cheo kwa huyo Mwenye Kiti cha Enzi, [20]
Anaye t'iiwa, tena muaminifu. [21]
Na wala huyu mwenzenu hana wazimu. [22]
Na hakika yeye alimwona kwenye upeo wa macho ulio safi. [23]
Wala yeye si bakhili kwa mambo ya ghaibu. [24]
Wala hii si kauli ya Shetani maluuni. [25]
Basi mnakwenda wapi? [26]
Haikuwa hii ila ni ukumbusho kwa walimwengu wote. [27]
Kwa yule miongoni mwenu anaye taka kwenda sawa. [28]
Wala nyinyi hamtataka isipo kuwa atake Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote. [29]