The Noble Qur'an Encyclopedia
Towards providing reliable exegeses and translations of the meanings of the Noble Qur'an in the world languagesDefrauding [Al-Mutaffifin] - Swahili translation - Ali Muhsen Al-Berwani
Surah Defrauding [Al-Mutaffifin] Ayah 36 Location Maccah Number 83
Ole wao hao wapunjao! [1]
Ambao wanapo jipimia kwa watu hudai watimiziwe. [2]
Na wao wanapo wapimia watu kwa kipimo au mizani hupunguza. [3]
Kwani hawadhani hao kwamba watafufuliwa . [4]
Katika Siku iliyo kuu! [5]
Siku watapo msimamia watu Mola Mlezi wa walimwengu wote? [6]
Hasha! Hakika maandiko ya wakosefu bila ya shaka yamo katika Sijjin. [7]
Unajua nini Sijjin? [8]
Kitabu kilicho andikwa. [9]
Ole wao siku hiyo kwa wanao kadhibisha! [10]
Ambao wanaikadhibisha Siku ya Malipo. [11]
Wala haikadhibishi ila kila mwenye kuruka mipaka, mwenye dhambi. [12]
Anapo somewa Aya zetu husema: Ni visa vya watu wa kale! [13]
Hasha! Bali yametia kutu juu ya nyoyo zao hao walio kuwa wakiyachuma. [14]
Hasha! Hakika hao siku hiyo bila ya shaka watazuiliwa na neema za Mola wao Mlezi. [15]
Kisha wataingia Motoni! [16]
Kisha waambiwe: Haya ndiyo mliyo kuwa mkiyakadhabisha. [17]
Hasha! Hakika maandiko ya watu wema bila ya shaka yamo katika I'liyyin. [18]
Na nini kitakacho kujuvya nini I'liyyin? [19]
Kitabu kilicho andikwa. [20]
Wanakishuhudia walio karibishwa. [21]
Hakika watu wema bila ya shaka watakuwa katika neema. [22]
Wakae juu ya viti vya enzi wakiangalia. [23]
Utatambua katika nyuso zao mng'aro wa neema, [24]
Watanyweshwa kinywaji safi kiliyo tiwa muhuri, [25]
Muhuri wake ni miski. Na katika hayo washindanie wenye kushindana. [26]
Na mchanganyiko wake ni Tasniim, [27]
Chemchem watakayo inywa walio kurubishwa. [28]
Kwa hakika wale walio kuwa wakosefu walikuwa wakiwacheka walio amini. [29]
Na wanapo pita karibu yao wakikonyezana. [30]
Na wanapo rudi kwa watu wao hurudi nao wamefurahi. [31]
Na wanapo waona husema: Hakika hawa ndio khasa walio potea. [32]
Na wao hawakutumwa wawe walinzi juu yao. [33]
Basi leo walio amini ndio watawacheka makafiri, [34]
Nao wako juu ya viti vya enzi wakiangalia. [35]
Je! makafiri wamelipwa malipo ya yale waliyo kuwa wakiyatenda? [36]