The Noble Qur'an Encyclopedia
Towards providing reliable exegeses and translations of the meanings of the Noble Qur'an in the world languagesThe Sundering, Splitting Open [Al-Inshiqaq] - Swahili translation - Ali Muhsen Al-Berwani
Surah The Sundering, Splitting Open [Al-Inshiqaq] Ayah 25 Location Maccah Number 84
Itapo chanika mbingu! [1]
Na ikamsikiliza Mola wake Mlezi, na ikapasiwa kumsikiliza! [2]
Na ardhi itakapo tanuliwa! [3]
Na kuvitoa vilivyo kuwa ndani yake, ikawa tupu! [4]
Na ikamsikiliza Mola wake Mlezi, na ikapasiwa kumsikiliza! [5]
Ewe mtu! Hakika wewe unajikusuru kwa juhudi kumwendea Mola wako Mlezi, basi utamkuta. [6]
Ama atakaye pewa daftari lake kwa mkono wa kulia! [7]
Basi huyo atahisabiwa hisabu nyepesi! [8]
Na arudi kwa ahali zake na furaha. [9]
Na ama atakaye pewa daftari lake kwa nyuma ya mgongo wake, [10]
Basi huyo ataomba kuteketea. [11]
Na ataingia Motoni. [12]
Hakika alikuwa furahani kati ya jamaa zake. [13]
Huyo hakika alidhani kuwa hatarejea tena. [14]
Kwani? Hakika Mola wake Mlezi alikuwa akimwona! [15]
Basi ninaapa kwa wekundu wa jua linapo kuchwa, [16]
Na kwa usiku na unavyo vikusanya, [17]
Na kwa mwezi unapo pevuka, [18]
Lazima mtapanda t'abaka kwa t'abaka! [19]
Basi wana nini hawaamini? [20]
Na wanapo somewa Qur'ani hawasujudu? [21]
Bali walio kufuru wanakanusha tu. [22]
Na Mwenyezi Mungu anajua wanayo yadhamiria. [23]
Basi wabashirie adhabu chungu! [24]
Isipo kuwa wale walio amini na wakatenda mema; hao watakuwa na ujira usio malizika. [25]