The Noble Qur'an Encyclopedia
Towards providing reliable exegeses and translations of the meanings of the Noble Qur'an in the world languagesThe Mansions of the stars [Al-Burooj] - Swahili translation - Ali Muhsen Al-Berwani
Surah The Mansions of the stars [Al-Burooj] Ayah 22 Location Maccah Number 85
Naapa kwa mbingu yenye Buruji! [1]
Na kwa siku iliyo ahidiwa! [2]
Na kwa shahidi na kinacho shuhudiwa! [3]
Wameangamizwa watu wa makhandaki. [4]
Yenye moto wenye kuni nyingi! [5]
Walipo kuwa wamekaa hapo! [6]
Na wao ni mashahidi wa yale waliyo kuwa wakiwafanyia Waumini. [7]
Nao hawakuona baya lolote kwao ila kuwa wakimuamini Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Msifiwa! [8]
Ambaye anao ufalme wa mbingu na ardhi; na Mwenyezi Mungu ni shaahidi wa kila kitu. [9]
Hakika walio wafitini Waumini wanaume na Waumini wanawake, kisha hawakutubu, basi watapata adhabu ya Jahannamu na watapata adhabu ya kuungua. [10]
Hakika walio amini na wakatenda mema watapata Bustani zenye mito ipitayo kati yake. Huko ndiko kufuzu kukubwa. [11]
Hakika kutesa kwa Mola wako Mlezi ni kukali. [12]
Yeye ndiye anaye anzisha na ndiye anaye rejeza tena, [13]
Naye ni Mwenye kusamehe, Mwenye mapenzi, [14]
Mwenye Kiti cha Enzi, Mtukufu, [15]
Atendaye ayatakayo. [16]
Je! Zimekuwasilia khabari za majeshi? [17]
Ya Firauni na Thamudi? [18]
Lakini walio kufuru wamo katika kukadhibisha. [19]
Na Mwenyezi Mungu nyuma yao amewazunguka. [20]
Bali hii ni Qur'ani tukufu [21]
Katika Ubao Ulio Hifadhiwa. [22]