The Noble Qur'an Encyclopedia
Towards providing reliable exegeses and translations of the meanings of the Noble Qur'an in the world languagesThe Dawn [Al-Fajr] - Swahili translation - Ali Muhsen Al-Berwani
Surah The Dawn [Al-Fajr] Ayah 30 Location Maccah Number 89
Naapa kwa alfajiri! [1]
Na kwa masiku kumi! [2]
Na kwa viwili viwili na kimoja kimoja! [3]
Na kwa usiku unapo pita! [4]
Je! Hapana katika haya kiapo kwa mwenye akili? [5]
Kwani hukuona jinsi Mola wako Mlezi alivyo wafanya kina A'di? [6]
Wa Iram, wenye majumba marefu? [7]
Ambao haukuumbwa mfano wake katika nchi? [8]
Na Thamudi walio chonga majabali huko bondeni? [9]
Na Firauni mwenye vigingi? [10]
Ambao walifanya jeuri katika nchi? [11]
Wakakithirisha humo ufisadi? [12]
Basi Mola wako Mlezi aliwapiga mjeledi wa adhabu. [13]
Hakika Mola wako Mlezi yupo kwenye mavizio anawavizia. [14]
Ama mtu anapo jaribiwa na Mola wake Mlezi, akamkirimu na akamneemesha, husema: Mola wangu Mlezi amenikirimu! [15]
Na ama anapo mjaribu akampunguzia riziki yake, husema: Mola wangu Mlezi amenitia unyonge! [16]
Sivyo hivyo! Bali nyinyi hamuwakirimu mayatima, [17]
Wala hamhimizani kulisha masikini; [18]
Na mnakula urithi kwa ulaji wa pupa, [19]
Na mnapenda mali pendo la kupita kiasi. [20]
Sivyo hivyo! Itakapo vunjwa ardhi vipande vipande, [21]
Na akaja Mola wako Mlezi na Malaika safu safu, [22]
Na ikaletwa Jahannamu siku hiyo, siku hiyo mtu atakumbuka! Lakini kukumbuka huko kutamfaa nini? [23]
Atasema: Laiti ningeli jitangulizia kwa uhai wangu! [24]
Basi siku hiyo hataadhibu yeyote namna ya kuadhibu kwake. [25]
Wala hatafunga yeyote kama kufunga kwake. [26]
Ewe nafsi iliyo tua! [27]
Rejea kwa Mola wako Mlezi umeridhika, na umemridhisha. [28]
Basi ingia miongoni mwa waja wangu, [29]
Na ingia katika Pepo yangu. [30]